Serikali
imeanza kupanga walimu wa sayansi moja kwa moja katika shule badala ya
Halmashauri kama ilivyokuwa awali ili kuleta uwiano sawa wa walimu
katika shule mbalimbali nchini.
Hayo
yamebainishwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Suleman
Jaffo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Muleba Prof. Anna Tibaijuka
lililohusu mkakati wa Serikali katika kukabiliana na tatizo la upungufu
wa walimu.
Naibu Waziri Jaffo amesema kuwa
Serikali imeandaa mkakati wa kuwaajiri wahitimu wa shahada za sayansi
ambazo siyo za ualimu baada ya kuwapa mafunzo ya muda mfupi kuhusu mbinu
za ufundishaji na maadili ya ualimu ili kukabiliana na changamoto ya
walimu wa sayansi nchini.
Naibu Waziri Jaffo amesema kuwa tayari kibali kimeombwa katika Ofisi ya Rais Utumishi kwa ajili ya utekelezaji huo, ambapo Serikali
imepanga kuajiri walimu wastaafu wenye uwezo wa kufundisha waliokuwa
wanafundisha masomo ya sayansi kwa mkataba ili kupunguza pengo lililopo.
Aidha,
Naibu Waziri Jaffo amebainisha kuwa Serikali inafanya tathimini ya
mahitaji ya walimu wa masomo ya sanaa kwa kila Halmashauri ili kubaini
maeneo yenye ziada na yenye upungufu ili kusawazisha.
“Mpango
wa Serikali uliopo ni kuwahamasisha walimu wa ziada wa masomo ya sanaa
kwenda kufundisha katika shule za msingi ndani ya Halmashauri husika,
ambapo kabla ya kuanza utekelezaji wa mabadiliko haya Serikali itatoa
waraka maalumu kwenda katika Halmashauri zote nchini” amefafanua Naibu Waziri huyo.
Akizungumzia
kuhusu utaratibu wa mafunzo ya walimu Mhe. Jaffo amesema kuwa
Halmashauri moja haiwezi kuwa na mfumo wa peke yake wa kuandaa walimu
hali ambayo iltakuwa ni vigumu kuthibiti ubora wa mafunzo hayo kwa
walimu.
Hata
hivyo amesema kuwa Serikali itaendelea kuongeza udahili wa walimu wa
sayansi katika vyuo vya ualimu kadri watakavyojitokeza ili kukidhi
mahitaji yaliyopo
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )