Wananchi
wameaswa kuwa wavumilivu na kuendelea kushirikiana na Serikali wakati
jitihada mbalimbali zikiendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na athari
za tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera hivi karibuni.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) George
Simbachawene alipokuwa akitoa kauli ya Serikali bungeni kuhusu Maafa
yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera siku ya
jumamosi tarehe 10/09/2016.
Waziri
Simbachawene amesema kuwa hadi leo tarehe 13/9/2016 idadi ya vifo
vilivyosababishwa na tetemeko hilo katika Mkoa wa Kagera ni 17, ambapo
majeruhi waliolazwa katika hospitali mbalimbali zilizoko Mkoani humo ni
169, majeruhi waliotibiwa na kuruhusiwa ni 83, nyumba za makazi
zilizoanguka ni 840, nyumba za makazi zenye nyufa ni 1,264 pamoja na
taasisi zilizoanguka na kupata nyufa ni 44.
Aidha,
Waziri Simbachawene amesema kuwa mpaka sasa Serikali imechukua hatua za
kuwaokoa watu na kuwapeleka hospitali kwa ajili ya matibabu na
kuwapatia makazi ya muda baadhi ya wananchi ambao nyumba zao
zimeathirika.
Pia
Serikali inaendelea kutibu majeruhi bure na wenye Bima za Afya kutumia
bima zao na kuongeza nguvu ya madaktari bingwa 15 kutoka mkoa ya Mwanza
ili kuweza kutoa huduma ya haraka kwa wahanga hao.
Vilevile
Waziri Simbachawene amesema kuwa Serikali imeelekeza wanajiolojia
kuwatoa hofu wananchi kwa kutoa maelekezo ya kisayansi kuhusu hali hiyo
na kuendelea kufanya tahimini ya athari zilizosababishwa na tetemeko
hilo.
Hata
hivyo Waziri Simbachawene amesema kuwa serikali imezifunga shule za
sekondari Ihungo na Nyakato zilizopo mkoani humo kutokana na athari za
tetemeko iliyopelekea kuharibika kwa miundombinu ikiwemo madarasa, vyoo,
mabweni na maabara, wakati serikali ikiendelea na taratibu za
kushughulikia tatizo hilo.
Waziri
Simbachawene ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa hatua
za dharura zinachukuliwa kwa kushirikiana na wadau wengine ili
kuhakikisha ili kuwasaidia wahanga.
Mbali
na hayo Mbunge wa Mlalo Mhe. Rashid Shangazi ametoa hoja juu ya wabunge
kuchangia posho yao ya siku moja ili iweze kuwasaidia wahanga wa
tetemeko hilo lililokadiriwa kuwa na ukubwa wa kiwango cha 5.7 katika
vipimo vya Richter ambapo wabunge waliunga mkono hoja hiyo na kuridhia
kuchangia kusaidia maafa hayo.
Aidha,
Mbunge wa Muleba, Prof. Anna Tibaijuka ameishukuru Serikali kuwepo
kwenye eneo la tukio mkoani Bukoba hatua ambayo imewapa faraja
wanakagera na kutoa wito kwa wabunge na watu wenye mapenzi mema kuzidi
kuwafariji wahanga hao.
Kwa
upande wake Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Charles Tizeba amesema
kuwa Serikali itafanya tathmini ya kina na ya kitaalamu ili kuepuka wale
ambao wanatumia maafa hayo katika kujinufaisha.
Akishukuru
kwa niaba ya Serikali Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
William Lukuvi amewashukuru wadau wote kwa kujitokeza na kushirikiana na
Serikali katika kutatua changamoto na kuwahakikishia wabunge kuwa
mchango wao utawafika walengwa na kuongeza kuwa jambo hilo limepelekea
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusitisha safari yake nchini
Zambia ili kuweza kusimamia suala hilo.
Aidha,
Waziri Lukuvi amesema kuwa Serikali inauchungu mkubwa juu ya maafa
hayo, hivyo amewataka wadau mbalimbali kujitokeza kusaidiana na Serikali
ili kuweza kuwasaidia wahanga hao na kuwapa pole waathirika wa
tetemeko hilo na kuwaombea marehemu wapumnzike kwa amani.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )