“Jioni
hii nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Mkuu wa
Mkoa Mstaafu Dkt. Joel Nkaya Bendera, natoa pole kwa familia yake na
wote walioguswa na msiba huu na pia naungana nao katika kipindi hiki cha
majonzi”
Hii
ni sehemu ya salamu za rambirambi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alizozitoa kufuatia kifo cha
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Joel Nkaya Bendera kilichotokea
jioni ya leo tarehe 06 Desemba, 2017 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
Jijini Dar es Salaam alikofikishwa kwa ajili ya kupata matibabu.
Mhe.
Rais Magufuli amesema Dkt. Joel Bendera atakumbukwa kwa mchango wake
mkubwa alioutoa kwa Taifa akiwa kiongozi katika nyadhifa mbalimbali
zikiwemo Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Naibu Waziri na Mbunge na pia kwa
mchango wake mkubwa katika maendeleo ya michezo.
“Dkt.
Joel Nkaya Bendera alikuwa kiongozi shupavu, mahiri na mchapakazi,
alipenda kufanya kazi kwa ushirikiano na daima alitamani kupata
mafanikio makubwa katika majukumu aliyokuwa nayo, hakika tutamkumbuka”
amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Pamoja
na kutoa pole kwa familia ya marehemu, Mhe. Rais Magufuli amewapa pole
wananchi wa Mkoa wa Manyara ambako alikuwa Mkuu wa Mkoa hadi tarehe 26
Oktoba, 2017, wananchi wa Mkoa wa Tanga ambako alikuwa Mbunge, wanachama
wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wanamichezo wote na wote walioguswa
na msiba huu na amemuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake
mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Desemba, 2017
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )