WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini zote kutumia nyumba za
ibada kuwahamasisha waumini wao umuhimu wa kulinda na kudumisha amani na
utulivu uliopo nchini.
Amesema
Serikali itahakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa nchini
ili Watanzania wawe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi zao za
kuwaingizia kipato na kuwaletea tija.
Waziri Mkuu ametoa wito huo jana
(Jumatatu, Septemba 12, 2016) wakati akizungumza na waumini wa dini ya
kiislam mara baada ya kumaliza kuswali sala ya Eid El Haji kwenye
viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke Dar es Salaam.
“Serikali
itaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote nchini. Wito wangu kwa
viongozi wa dini msisitize waumini juu ya utunzaji wa amani pamoja na
kukemea vitendo viovu ili Taifa lizidi kusonga mbele,” amesema.
Wakati
huo huo Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi kuendelea kuwaombea mahujaji
waliopo mjini Makka na Madina nchini Saudi Arabia wakiendelea na ibada
ya hijja warudi salama.
Pia
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kuwasaidia kwa hali
na mali watu waliokumbwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera ambako jumla
ya watu 16 walifariki na wengine 253 kujeruhiwa.
Pia
maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na
nyingine 1264 zikipata nyufa yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali
za umma
Awali
akisoma hutuba ya Eid viwanjani hapo Sheikh Nurdin Kishki alisema dini
ya Uislamu ni dini ya amani hivyo amewaomba waislamu kujiepusha na
vitendo vya uvunjifu wa amani yakiwemo mauaji ya watu wasiokuwa na
hatia.
Sheikh
Kishki amesema ni muhimu watu kulinda amani kwani ikitoweka ni vigumu
kuirudisha, alitolea mfano wanachi wa nchi za Libya na Misri ambazo hadi
sasa zimeshindwa kuirudisha.
Amesema
mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya uwamwagaji wa damu, kudhulumu
mali za watu pamoja na kuwavunjia heshima wenzake atakuwa ameangamia,
hivyo amewataka Watanzania hususan wakazi wa Temeke kujiepusha navyo.
“Temeke
sasa inaongoza kwa matukio ya mauaji, wanaua hadi walinzi. Askari
wameuawa bila hatia, jambo hili linasikitisha sana. Watu waliokuwa
wanafanya kazi ya kulinda raia na mali zao wanauawa bila ya hatia!
Ameongea kwa masikitiko na kuwaomba Watanzania wajiepuszhe na vitendo
hivyo.
Katika
hatua nyingine Sheikh Kishki ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa
kuonyesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kuwaletea
maendeleo hivyo amewaomba wananchi wawe mstari wa mbele kutoa
ushirikiano ili taifa liweze kusomba mbele.
“Ndugu
zangu tumepewa heshima kubwa leo kuswali Eid na Mheshimiwa Waziri Mkuu
tena amekuja hapa kwenye viwanja hivi vya Mwembe Yanga, hii inaonyesha
ukaribu wa viongozi wetu wakuu kwa wananchi wao hususan wa hali ya
chini,” amesema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUUTupe Maoni Yako( Matusi Hapana )