Lukuvi ameeleza hayo wakati akihojiwa katika kipindi cha ‘KUMEKUCHA’ kinachorushwa na kituo cha runinga cha ITV.
“Mtu akinunua ardhi hupewa karatasi za ofa ambazo hivi sasa zilizojaa ni feki, lakini wapo wajanja na matapeli wanatumia ofa hizo kudhulumu viwanja vilivyo wazi. Mfano wakiona kiwanja kipo wazi wanakwenda katika halmashauri wanashirikiana na baadhi ya maafisa ardhi wasio waaminifu, wanauliza namba ya ploti ya kiwanja husika na anayemiliki,” alisema.
“Wakishajua namba na mmiliki wa kiwanja huiondoa ofa halali katika faili kisha afisa ardhi anaiweka feki, siku mmiliki halali akienda kuulizia kiwanja chake katika halmashauri anakuta ofa yake haipo ipo ya mtu mwingine ambaye ameghushi tarehe ya barua ya ofa,”aliongeza.
Aidha Lukuvi alisema matapeli wa ardhi huyafahamu maeneo yaliyo wazi na kwamba asilimia kubwa hushughulika na yale ambayo wamiliki wake wamefariki dunia.
“Hawa matapeli huyajua maeneo vizuri, na wanachokifanya ni kutengeneza ofa feki kisha kuziweka katika faili za halmashauri, ukienda mmiliki halali unaambiwa ni tapeli kwa kuwa barua yako haiko katika faili,” amesema na kuongeza,”Matapeli wanaishi mjini kwa kutengeneza ofa bandia, wastaafu,yatima na wajane wanalizwa kila siku,” amesema.
Ametoa agizo kwa maafisa ardhi wa kanda kutotoa huduma wala kushugulika na barua za ofa kwa sababu baadhi yao ndio wanaobadilisha ofa halali za watu.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )