
TANGU mwaka huu uanze kumekuwa na matukio mengi yaliyojitokeza kwa
mastaa, ambayo yalileta mshtuko kwenye jamii hususan kwa watu
wanaofuatilia masuala ya burudani kwa wasanii, hapa nakuorodheshea
matukio hayo.
1.MAKONDA KUWATUMBUA MASTAA ISHU YA DAWA ZA KULEVYA Ni ishu iliyokuwa
gumzo jijini kufutokana na Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda kuwatumbua
baadhi ya wasanii kwa kuwataja majina na kuwaita Kituo Kikuu cha Polisi
kutokana na kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya. Miongoni mwa
wasanii waliokuwepo kwenye orodha hiyo ni Wema Sepetu, Lulu Abbas ‘Lulu
Diva’, Recho kizunguzungu, TID, Petitman, Deogratius Shija, Salma Jabu
Nisha, Tunda Sebastian na wengine wengi.

2.WEMA KUHAMA CHAMA Mwanadada huyu alikuwa mstari wa mbele kwenye Chama
Cha Mapinduzi (CCM), hususan kwenye kampeni ya ‘mama ongea na mwanao’
ambayo ilikuwa ikiendeshwa katika kipindi cha uchaguzi, wakimsapoti
Makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan. Lakini ghafla baada ya Wema
kupata msala wa kutumia dawa hizo alihama chama hicho na kuhamia Chadema
kwa kuhisi CCM ilimtenga baada ya kupata tatizo hilo.
3. NAY KUWEKWA NDANI Ilikuwa kizaazaa pale mwanamuziki Emanuel Elibarick
alipowekwa ndani baada ya kutoa wimbo uitwao Wapo ambao ulionekana
kuwakashifu baadhi ya viongozi wa kiserikali. Hata hivyo, ilikuwa ni
kauli moja tu ya Rais Dk John Magufuli aliyesema aachiwe na ikawa hivyo.
Mwanamuziki huyo alikaa ndani siku moja.
4.ROMA KUTEKWA Nchi nzima ilizizima kutokana na mwanamuziki wa Hip Hop,
Ibrahimu Mussa ‘Roma Mkatoliki’ kutekwa pamoja na mwanamuziki Moni
Central Zone na kijana mwingine ambaye alikuwepo studio hapo Tongwe
Record, gumzo hilo liliendelea hadi walipopatikana huku kila mmoja
akizungumza lake kuhusu nani alifanya utekaji huo.
5. NUH KUACHANA NA NAWAL Wengi hawakuamini kilichotokea wakawa wanahisi
ni kiki baada ya mwanamuziki Nuh Mziwanda kubwagana na mkewe Nawal
ambaye amebahatika kupata naye mtoto mmoja Anya. Lakini huo ndiyo
ulikuwa ukweli maana baadaye mwanadada huyo alifunga ndoa na mtu
mwingine.

6. HARUSI YA JOTI Taarifa za harusi hiyo zilipoanza kuenea watu
walifikiri ni utani. Lakini baadaye Joti na mkewe walipoonekana wakiwa
kanisani na picha kutoka vikiwemo vipande vya video huku mitandao ya
kijamii ikienea habari zake, kila mmoja aliamini kweli Joti amefunga
ndoa na mkewe.
7. BIFU LA HAMISA NA ZARI Hili ni miongoni mwa matukio yaliyobamba mwaka
huu. Bifu hili liliibuka baada ya mwanamitindo Hamisa Mobeto kuweka
wazi kwamba alizaa na Mbongo Fleva ambaye ni mzazi mwenza na
mjasiriamali Zarinnah Hassan ‘Zari Ze Bossy Lady.” Hata hivyo, baada ya
vijembe mitandaoni baadaye suala hili lilionekana la kawaida na kupitwa
na wakati.
8. NDOA YA UWOYA NA DOGO JANJA Taarifa za muigizaji Irene Uwoya kufunga
ndoa na Mbongo Fleva, Dogo Janja ziliwashangaza wengi. Ikawa gumzo kubwa
ambalo baadaye lilikosa tija baada ya Uwoya kuweka wazi kupitia
magazeti ya Global Publishers kwamba hakufunga ndoa bali ni muvi
inayotarajiwa kutoka.

9. LULU KUTUPWA JELA Tukio la muigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’
kuhukumiwa kwenda jela kwa muda wa miaka miwili kutokana na kesi ya
kumuua bila kukusudia muigizaji Steven Kanumba ilikuwa ni gumzo mpya
kwenye media (vyombo vya habari). Wengi hawakuamini kama Lulu angeweza
kwenda jela, lakini sheria ni msumeno na hivi tunavyozungumza Lulu yupo
jela Seregea.
10. DK SHIKA NA ITAPENDEZA Hadi sasa hili ndilo tukio la funga mwaka.
Tukio hili limebamba baada ya kuibuka mzee mmoja aliyevaa nguo za
kawaida na sandozi zilizochoka mguuni akitaka kununua nyumba za Saidi
Lugumi. Mzee huyo si mwingine bali Dokta Loius Shika ambaye alijizolea
umaarufu kwenye mnada huo na msemo wa ‘mia tisa itapendeza’ na kuweka
wazi kwamba ana mabilioni ya pesa kwenye benki tofauti tofauti nje ya
nchi, kwa sasa mzee huyo anakula madili ya matangazo likiwemo kutoka
Kampuni ya Sokabet.
CHANZO JIACHIE
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )