Makamu
wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd amesema ushauri wa
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutaka kuongezwa muda wa urais kutoka
miaka mitano mpaka miaka saba ni suala zuri na linazungumzika bila
matatizo.
Balozi
Idd aliyasema hayo jana wakati akifunga mkutano wa nane wa Baraza la
Tisa la Wawakilishi lililochukua muda wa wiki moja mjini hapa.
Awali
baadhi ya wajumbe wa baraza hilo wakichangia Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Tume ya Uchaguzi ya mwaka 1984 na kuweka sheria ya mwaka
2017, walisema kuwa ili Zanzibar iepukane na matumizi hasa kipindi cha
uchaguzi hakuna budi kuongezwa kwa muda wa utumishi wa urais.
Mmoja
wa wawakilishi hao wa Jimbo la Shaurimoyo, Hamza Hassan Juma amesema
kuwa ili kumpa Rais wakati mzuri wa kutumikia wananchi ipasavyo hakuna
budi muda wake kuongezwa zaidi ili lengo la kufikisha maendeleo kwa
wananchi liweze kufanikiwa.
Alisema
kwa kuwa muda wa miaka mitano ya uongozi wa rais madarakani linaonekana
kupoteza fedha nyingi za wananchi kwa kufanya uchaguzi kila baada ya
miaka mitano, ni vyema uongozi ukaliona hilo na kulifanyia kazi.
Alisema
kwa mujibu wa tathmini yake ya uchaguzi mkuu mara nyingi hutumia fedha
nyingi za walipakodi kiwango ambacho kinaweza hata kujenga zaidi ya
shule kubwa 20 ambazo zingeisaidia jamii kuondokana na uhaba wa shule.
Alisema
kuwa pamoja na katiba zote mbili ya Tanzania Bara na Zanzibar kuweka
muda huo wa miaka mitano, bado kuna nafasi kubwa kwa Zanzibar kufanya
marekebisho ya katiba yao ili kuongeza muda, akidai kuwa ni jambo ambalo
haliwezi kuathiri hata kidogo Katiba ya Tanzania.
Juma
alisema ikiamuliwa kufanyika hivyo ni wazi kuwa faida kubwa inaweza
kupatikana ikiwamo Rais kupata muda mwingi wa kutumikia jamii badala ya
muda wa sasa wa miaka mitatu tu ya kutumia jamii huku miaka miwili
iliyosalia akishughulikia masuala ya uchaguzi.
Balozi
Iddi akitolea ufafanuzi suala hilo alisema kwa kuwa jambo hilo
linahusiana na pande mbili za Muungano ni vema kwa wakati huu suala hilo
likaachiwa kwa viongozi husika kwa kulifanyia kazi na ikionekana
linafaa ni wazi linaweza kupunguza gharama kubwa hasa kwa upande wa
chaguzi za viongozi wakuu.
“Hili
itakuwa si suala jipya kwetu kwani hata ndugu zetu wa Rwanda nao
wameongeza muda wa uongozi, hivyo nasi tukibadili miaka badala ya mitano
tukaweka saba tunaweza kufanikiwa kimaendeleo kwa hatua kubwa,” amesema
Balozi Idd.
Alisema
hali hiyo pia inaweza kuleta mafanikio makubwa katika chaguzi zijazo
kufanyika kwa ufanisi mkubwa hasa baada ya marekebisho ya sheria ya
uchaguzi yaliyofanyika.
Alisema
Serikali ipo tayari na itaendelea kila mara kuwa hivyo kwa kupokea
michango mbalimbali ya wawakilishi ambayo inaonekana inafaa kwa ajili ya
kujenga maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Hata
hivyo, Balozi Iddi akifunga mkutano huo alisema kuwa Serikali
imedhamiria kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi wake ili
kuona nao wanaishi katika hali ya matumiani.
Alisema
kuwa miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali tayari wameanza
kununua meli moja ya mafuta, huku harakati za ununuzi wa meli kwa ajili
ya abiria zikiendelea kutoa matumaini.
“Meli
hizi kwa ufupi zinaweza kusaidia harakati za wananchi wetu hasa kwa
kuwa na usafiri wa uhakika ambao utasaidia katika upatikanaji wa huduma
mbalimbali,” alisema Balozi Idd.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )