Akizungumza
wakati wa kuaga miili ya askari 14 waliofariki katika mapigano na waasi
wa kikundi cha ADF nchini DRC, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema
Serikali inataka baada ya uchunguzi huo hatua zichukuliwe ili kutenda
haki.
Miili
ya askari hao imeagwa leo Alhamisi, Desemba 14,2017 katika viwanja vya
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa jijini Dar es Salaam.
“Serikali
ya Tanzania inataka Umoja wa Mataifa ufanye uchunguzi wa kina, ulio
wazi na wa ukweli kwa damu hizi za Watanzania zilizomwagika ili tujue na
haki iweze kutendeka. Ni matumaini yetu kuwa Umoja wa Mataifa watafanya
hivyo kwa haraka,” amesema.
Majaliwa
ameishukuru Serikali ya DRC na UN kwa ushirikiano baada ya kutokea
shambulizi hilo. Amewataka Watanzania waungane kuwaombea mashujaa hao na
kuenzi mchango wao kwa Taifa.
Amesema
Tanzania imekuwa ikishiriki ulinzi wa amani sehemu nyingi kama vile
Lebanon, Darfur na DRC na maeneo yote wanapokuwepo askari wa Tanzania
wanasifiwa kwa ufanisi wa kazi.
“Msiba
huu ni wa Taifa lote na watu wote wenye kupenda amani, daima
tutawakumbuka mashujaa wetu na kuendelea kuenzi na kujivunia kazi zao na
mchango wao mkubwa kwa nchi yetu na duniani kwa jumla,” amesema.
Waziri
Mkuu Majaliwa ameliambia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwamba,
yaliyotokea DRC yasiwakatishe tamaa katika kutimiza wajibu wao nchini
humo na kwingineko ambako wanatekeleza majukumu yao ya ulinzi wa amani.
Awali,
akizungumza wakati wa kuaga miili ya askari hao, Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo alisema askari hao waliuawa kwenye
mapigano yaliyodumu kwa saa 13.
Amesema
majeruhi wa shambulio hilo linalodaiwa kufanya na waasi wa ADF
wanaendelea vizuri na wanapatiwa matibabu katika hospitali zilizopo
Goma, Kinshasa na wengine wamepelekwa Uganda.
Shughuli
ya kuaga miili ya mashujaa hao imehudhuriwa na viongozi kadhaa
wakiwemo, Rais mstaafu Jakaya Kikwete na mkewe Salma; wakuu wa majeshi
wastaafu Robert Mboma, Mirisho Sarakikya na Davis Mwamunyange; Waziri
Mkuu mstaafu Mizengo Pinda; mawaziri, wabunge na wawakilishi wa Umoja wa
Mataifa.
Miili ya askari hao ilirejeshwa nchini kwa ndege ya Umoja wa Mataifa Desemba 11,2017.
Jumapili
Desemba 10, 2017 Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali James
Mwakibolwa alisema askari hao walivamiwa kambini na waasi wa ADF na
mapigano yalidumu kwa takriban saa 13. Alisema askari 14 wa JWTZ
waliuawa, 44 walijeruhiwa na wengine wawili hawajulikani walipo.
Taarifa iliyotolewa baadaye na jeshi ilisema askari mmoja amepatikana.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )