Mtangazaji wa Azam TV na mmiliki wa MPENJA BLOG,
Baraka Adson Mpenja (kulia) akieleza kwa kifupi tathmini ya mechi ya
Yanga v Coastal Union kabla ya kumhoji mfungaji wa magoli manne (4) kati
ya 8, Amissi Tambwe
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Tambwe ameifungia Simba SC mabao
21 katika Ligi Kuu Tanzania, 19 akiyafunga msimu uliopita na mawili
msimu huu kabla ya kutimkia Yanga SC dirisha dogo.'
BAADA ya kuwa na wakati mzuri ndani ya kikosi cha Yanga SC, mshambuliaji
Amisi Tambwe, amesema hafikirii kurejea mtaa wa Msimbazi jijini hapa
kuitumikia kwa mara ya pili Simba SC.
Katika mahojiano na mtandao huu jijini hapa leo, Tambwe, mchezaji wa
zamani wa Vital'O ya kwao Burundi, amesema anajisikia vyema kucheza
ndani ya kikosi cha Mdachi Hans van der Pluijm cha Yanga SC.
Amesema taarifa zinazoenezwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba ana
mpango wa kurejea Simba SC baada ya msimu huu kumalizika si za kweli.
"Sifikirii kurudi Simba. Mimi ni mchezaji wa Yanga na ninajisikia vizuri
kuwa hapa. Nimefunga magoli tisa ligi kuu na mawili katika michuano ya
kimataifa. Ni jambo jema kwangu na klabu ya Yanga pia," amesema Tambwe.
Aidha, straika huyo ambaye msimu huu amefunga mabao saba kwa kichwa na
manne kwa mguu (matatu mguu wa kulia) katika mashindano yote akiwa na
Simba SC na Yanga SC, amesema mabao yake manne katika mechi ya jana
yamerejesha matumaini kutetea kiatu chake cha dhabu cha zawadi ya
mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Bara msimu huu.
Tambwe alifunga mabao manne Yanga ilipowanyanyasa mabingwa wa 1988 wa
Tanzania Bara, Coastal Union FC Uwanja wa Taifa jijini hapa jana ikiwa
ni hat-trick yake ya tatu Ligi Kuu ya Bara tangu aanze kukipiga Tanzania
msimu uliopita.
Ilikuwa mara ya pili kwa mshambuliaji huyo pia kufunga mabao manne pekee
yake katika mechi moja baada ya kufanya hivyo pia katika ushindi wa
mabao 6-0 wa Simba dhidi ya Mgambo Shooting Stars Uwanja wa Taifa jijini
hapa msimu uliopita.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )