Polisi mmoja anadaiwa kumpiga risasi dereva daladala, Pistus Ngowi baada ya kutofautiana kauli.
Tukio
hilo lililotokea juzi saa tatu usiku, Kariakoo jijini Dar es Sallam
lilisababisha madereva wenzake wanaofanya wote safari za Tandika pamoja
na wa Temeke kugoma kwa zaidi ya saa tano wakidai kwamba licha ya
kushambuliwa, amebambikiwa kesi katika Kituo cha Polisi cha Msimbazi.
Ilidaiwa
kuwa wakiwa katika Mtaa wa Lindi kilipo kituo cha daladala hizo, polisi
huyo aliyetajwa kwa jina moja la Dotto akiwa kwenye doria,
walitofautiana na dereva huyo kisha kumtolea bastola na kumpiga nayo
mkononi.
Kamanda
wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jana kuwa
awali, alipewa taarifa za askari wake kushambuliwa akiwa doria na
alimpiga risasi dereva huyo kujitetea.
“Huyu askari yupo mahabusu anahojiwa na polisi ili kubaini chanzo cha tukio hili,”alisema Kamanda Sirro.
Dereva
wa daladala aliyeshuhudia tukio hilo, Mateso Elias alidai kuwa walikuwa
madereva 15, waliokuwa wakisubiri abiria ghafla walisikia kelele za
Dotto akimfokea dereva huyo akidai kuwa alitaka kumgonga alipokuwa
akiwasili kituoni hapo.
Alisema
ili kuepusha shari, Ngowi alishuka kwenye basi na kumuomba msamaha
akiwa amepiga magoti lakini polisi huyo alikataa kumsamehe.
Alisema kitendo hicho kiliwavuta madereva waliokuwapo hapo ambao walisogea eneo hilo kujua kilichokuwa kinaendelea: “Ghafla
alitoa bastola na kutuamuru wote tuondoke. Tulipopiga hatua kama hatua
tano, alifyatua risasi na kumpiga Ngowi mkononi na nyingine alipiga
hewani.”
Alisema baada ya tukio hilo aliwapigia simu askari wenzake ambao walifika na kumpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )