Waziri
wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe leo amemsimamisha kazi
mkurugenzi mtendaji wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Juma Mgoo pamoja
na vigogo wengine wawili kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya uvunaji
wa kasi wa misitu pamoja na usafirishaji wa magogo.
Wakurugenzi
wengine waliosimamishwa kazi leo ni pamoja na Zawadi Mbwambo (Mratibu
wa Maliasili) na Nurdin Chumuya (Mipango na Matumizi ya Rasilimali).
Kwa upande mwingine, Prof
Maghembe amemfuta kazi mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Wanyamapori Dk
Charles Mulokozi kwa kuwezesha upatikanaji wa kibali cha kuwasafirisha
nyani wekundu 61 kwenda Albania huku uchunguzi ukionyesha badala ya idadi hiyo, wanyama kama hao 300 walikamatwa pasipo kibali cha uwindaji.
Kwa
mujibu wa waziri huyo, ripoti ya ukaguzi uliofanywa na TFS, imebainika
ukiukwaji mkubwa hususani katika makusanyo ya mapato na uvunaji magogo
usiozingatia sheria za nchi.
Amebainisha
kuwa, wakati mwingine watendaji wa misitu walikuwa wakidanganya juu ya
mapato halisi yaliyokuwa yanapatikana katika sekta ya misitu.
“Inapofikia
wakati unakusanya mapato na ama kupeleka benki pungufu au kutopeleka
kabisa kwa zaidi ya mwaka na wakati mwingine taarifa za kibenki
zinakinzana ….hii ni aibu kubwa sana,” Waziri Maghembe amesema.
Profesa
Maghembe amesema ripoti hiyo imefichua kuwa mkoa wa Rukwa unaongoza kwa
uvunaji haramu wa magogo hususani wilayani Kalambo.
“Walichokuwa
wanakifanya ni kwamba baada ya uvunaji, magogo yalikuwa yakipelekwa
Zambia na kurudishwa Tanzania tena ili kudanganya kuwa magogo hayo
yamevunwa nchini Zambia.
“Niliwasiliana na maofisa wa juu wa TFS na nilisubiri wachukue hatua lakini hakuna kilichofanyika,” kwa hasira waziri Maghembe amesema.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )