Tunapoelekea
kipindi hiki cha sikukuu ya Pasaka ambayo inaanza kesho Ijumaa Kuu,
Jeshi la Polisi nchini, linatoa tahadhari kwa wananchi, kuwa makini
katika suala zima la ulinzi na usalama wa maisha na mali zao.
Katika kipindi cha sikukuu baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo vya uhalifu.
Hata
hivyo, Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kwa kushirikiana na vyombo
vingine vya ulinzi na usalama katika mikoa yote kuhakikisha kwamba
hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza na pale
vitakapojitokeza vitadhibitiwa kwa haraka.
Ulinzi
umeimarishwa kwenye maeneo yote, yakiwemo maeneo ya kuabudia, fukwe za
bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo yatakuwa na
mikusanyiko mikubwa ya watu.
Aidha,
Jeshi la Polisi halitasita kumuwajibisha mzazi ama mlezi yeyote
atakayeshindwa kutunza mtoto wake na kusababisha mtoto huyo kupotea au
kupata madhara.
Pia
tunawataka wananchi wote kuwa wepesi katika kutoa taarifa pindi
wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo yao ya makazi ama
maeneo ya biashara. Simu za polisi endapo mwananchi atakuwa na taarifa
ni 111 au 112.
Vilevile,
Jeshi la polisi linawataka wananchi kuwa makini na watu wanaojipatia
kipato kwa njia za utapeli kwa kutumia simu na mitandao.
Mtu
yeyote asikubali kutaja taarifa zake binafsi kwa mtu asiyemjua,
mfano kutaja namba ya siri ya akaunti anayotumia kuhifadhia pesa
katika simu, ama kutuma pesa kwa mtu ambaye huna uhakika naye.
Jeshi
la Polisi linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia
barabara kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa
kwa madereva wa magari na pikipiki, kuepuka kujaza watu kupita kiasi,
kubeba mishikaki, kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi pamoja na kupiga
honi hovyo.
Tunawatakia watanzania wote Pasaka njema.
Imetolewa na:
Advera Bulimba -SSP
Msemaji wa Jeshi la PolisiTupe Maoni Yako( Matusi Hapana )