Featured
Loading...

Mwandishi Salma Said Apatikana Baada ya Watekaji Kumuachia Huru


Siku tatu baada ya mwandishi wa Mwananchi na DW, Salma Said kutoweka, jana alipatikana baada ya kukutwa katika Hospitali ya Regency ya jijini Dar es Salaam  na kupelekwa kituo kikuu cha polisi kuhojiwa.
Habari zilizopatikana jana jioni na kuthibitishwa na mumewe, Ali Salim Khamis na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi, Simon Siro zilisema Salma alisajiliwa jana mchana katika hospitali hiyo.
Ali aliyekuwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, alisema kwa ufupi kuwa amepata taarifa hizo na kufika Dar es Salaam kuzifuatilia. 
Kamanda Siro alisema ni kweli Salma amepatikana na ametumwa mkuu wa upelelezi wa kanda hiyo kumfuata hospitali ampeleke kituoni kwa mahojiano. 
“ Tumefungua jalada la uchunguzi wa tukio hili juzi,” alisema Sirro na kuongeza. 
“Wapelelezi walizungumza na mume wa Salma na kuna mambo amewaeleza lakini hatuwezi kuyaweka wazi kwa sasa, hadi uchunguzi utakapokamilika, tumeipata namba ya simu aliyowasiliana nayo na mumewe akiwa huko kunakoaminika amefichwa,” alisema. 
Wakati huo huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika tamko lake ililolitoa jana ilieleza kuwa kutekwa kwa mwanahabari huyo kumezua maswali mengi kwa wananchi, familia yake, wadau na wanahabari wa ndani ya nchi na wale wa jumuia za kimataifa.
“Kutekwa kwa Salma kunatokana na kazi yake ya uanahabari, ndiyo maana ushahidi wa awali uliopatikana kwa njia ya ujumbe wa sauti ukiwa na sauti inayoaminika kuwa ni yake, ulieleza wazi kutekwa kwake kunatokana na yeye kuripoti dosari zinazoendelea katika uchaguzi wa marudio Zanzibar,” alisema Joseph Mbilinyi, Waziri Kivuli wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo wa Kambi ya Upinzani. 
Mbilinyi ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema) alidai kuwa matukio mbalimbali yanayoendelea Zanzibar yakiwamo ya matumizi ya nguvu, vitisho na hata vitendo vya kikatili dhidi ya wanaosimamia haki, vinaendelea kuitia Serikali ya CCM doa, Taifa na dunia nzima.

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top