Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezifungia kurasa za facebook na tovuti
ya www.focusvikoba.wapka.mobi baada ya kugundua kuwa zinatumia majina
ya viongozi kutapeli watu.
Mkurugenzi
Mkuu wa TCRA, Dk Ally Simba aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa,
matapeli wanaofanya uhalifu huo wametumia majina ya Janet Magufuli,
ambaye ni mke wa Rais na Samia Suluhu ambaye ni Makamu wa Rais
kufanikisha utapeli wao.
Dk
Simba alisema mamlaka yake imegundua kuwa wahalifu hao wa mtandao
huanzisha tovuti, kurasa za facebook na blogu kwa kutumia majina ya
viongozi wakuu wa nchi ili kujipatia fedha kutokana na umaarufu wa watu
hao.
Alisema
matapeli hao hutumia mitandao hiyo kuwadanganya wananchi kuwa kuna
fursa za kupata mikopo au misaada kupitia vikundi vya kusaidiana,
maarufu kwa jina la vikoba.
“Kwa
mfano kuna matapeli walioanzisha ukurasa wa mtandao wa kijamii wa
facebook kwa jina la mke wa Rais, Mama Janet Magufuli na kwa jina ma
Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan wakilenga kujipatia kujipatia
fedha,” alisema Dk Simba.
Aliongeza
kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya
Mwaka 2015, mtu yeyote haruhusiwi kujitambulisha kwenye mitandao kwa
kutumia utambulisho wa mtu mwingine.
Alisema
adhabu ya kosa hilo imeainishwa kwenye kifungu cha 15(2) kinachosema
anayepatikana na hatia anaweza kutozwa faini isiyopungua Sh5 milioni au
mara tatu ya thamani ya kile atakachokuwa amekipata kupitia utapeli.
Aliwataka
wananchi kuwa macho dhidi ya mitandao ya kijamii, tovuti na blogu
ambazo zinawataka kutuma fedha au kuchangia kitu chochote ili wapewe
mikopo au misaada.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )