Featured
Loading...

Vodacom, Tigo, Airtel, Smart na Zantel Zapigwa Faini ya Mamilioni ya Pesa Na TCRA Kwa Kutoa Huduma Mbovu za Mawasiliano

Kufuatia malalamiko kuhusu huduma duni za mitandao ya simu nchini, Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) imezitoza faini kampuni kwa kushindwa kuwajibika katika huduma zao.

Kampuni za simu zilizopigwa faini kutokana na kutoa huduma mbovu ni pamoja na Airtel, Smart, Tigo, Vodacom na Zantel. Pamoja na hivyo, zimetakiwa kuboresha huduma zake ndani ya miezi sita.

TCRA imefanya tathimini juu ya ubora wa huduma za mawasiliano ikiwemo sauti na data zinazotolewa na kampuni hizo ambapo imebainika kutowatendea haki watumiaji wake.

“TCRA inazipiga faini kampuni hizi zinazoanzia milioni 12.5 mpaka milioni 27.5 na inazitaka kuboresha huduma zao, miezi sita tangu siku ya kutolewa kwa tangazo hili,” imeeleza sehemu ya taarifa ya TCRA kwa vyombo vya habari.

Usumbufu unaotajwa na TCRA ambao unafanywa na mitandao hiyo ni pamoja na kudai namba haipatikani ilihali ipo hewani, kudai namba inatumika ilihali sivyo, kukata salio la mteja pasipo ridhaa yake na kukatika kwa mawasiliano mara kwa mara.

Kampuni ya Vodacom ndiyo iliyopigwa faini kubwa zaidi (milioni 27.5) huku Kampuni ya Smart ikipigwa faini ndogo zaidi (milioni 12.5), faini hizo zimetozwa kulingana na ukubwa wa makosa ambayo kampuni husika imekuwa ikiyafanya katika utoaji wa huduma zake.

Kampuni ya Airtel imepigwa faini ya Sh. 22.5 milioni, Zantel Sh. 25 milioni na Tigo Sh. 25 milioni. TCRA imezitaka kampuni hizo kulipa faini hizo haraka iwezekanavyo na kuboresha huduma zao kabla ya mamlaka hiyo kuchukua hatua kali zaidi.

Kwa mujibu wa kifungu cha 17 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Sura ya 306 mamlaka hiyo hapa nchini inayo mamlaka ya kutoa adhabu kwa kampuni yoyote inayokiuka masharti ya leseni ya utoaji huduma.

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top