Featured
Loading...

Waziri Anayefaidi Posho za Magufuli Huyu Hapa...

Wakati amri ya Rais John Magufuli ya kufuta safari zote za nje ya nchi kwa watumishi wa umma ikiendelea kushika kasi, imebainika kuwa hadi sasa ni waziri mmoja tu ndiye walau amefanikiwa kwenda nje ya nchi baada ya kukidhi vigezo vilivyopo.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe, umebaini kuwa waziri huyo mwenye bahati ya pekee hadi sasa ni Balozi Augustino Mahiga wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
Katika agizo lake alilolitoa siku chache baada ya kuingia madarakani Novemba 5, Rais Magufuli alisema ni marufuku kwa kiongozi au mtumishi yeyote wa umma kwenda nje ya nchi bila ya kupata kibali kutoka kwake au kwa Katibu Mkuu Kiongozi – Ikulu.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa ili kiongozi au mtumishi yeyote wa umma apate kibali cha kusafiri kwenda nje ya nchi, ni lazima aeleze wazi kuwa safari hiyo anayotaka kwenda ina manufaa gani kwa taifa na kwamba, ni athari zipi zitatokea kwa taifa iwapo safari hiyo haitafanyika.
Uchunguzi umebaini kuwa tangu kutolewa kwa agizo hilo, ni Balozi Mahiga pekee ndiye aliyemudu kukidhi vigezo vya safari na hivyo kupata fursa ya kufaidi posho zianzoambatana na safari za aina hiyo ambazo Rais Magufuli anazipinga vikali kwa maelezo kuwa huligharimu taifa mabilioni ya fedha ambayo yangeweza kutumika kwa shughuli nyingine za maendeleo.
Katika hotuba yake wakati akizindua Bunge Novemba 20, 2015, Rais Magufuli alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2013/2014 na 2014/2015, taifa lilitumia zaidi ya Sh. bilioni 356.3 kwa ajili ya kugharimia safari za nje; jambo ambalo kamwe yeye hatakubali litokee kwa sababu fedha hizo zinaweza kukamilisha miradi mingi ya maendeleo ikiwamo kujenga barabara ya lami ya urefu wa kilomita 400.
“Kwakweli hali ni mbaya. Safari za Ulaya, Marekani na kwingineko nje ya nchi ndizo zilizokuwa zikitumiwa na mawaziri na vigogo wengine wa taasisi za umma kuvuna utajiri kupitia manunuzi ya tiketi na posho… hivi sasa anayenufaika ni Waziri Mahiga tu ambaye twaweza kusema ana bahati sana kwa sababu wizara yake haiwezi kukwepa safari,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe.
Wakati wa utawala wa awamu ya nne, mawaziri walikuwa wakisafiri mara kwa mara, katika kile ambacho aliyekuwa waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliwahi kukaririwa akisema kuwa ‘walikuwa wakipishana angani utafikiri nyumbani kunawaka moto’.
Chanzo kingine kiliiambia Nipashe kuwa kabla ya kuingia Ikulu kwa Magufuli, kuna mawaziri walikuwa wakivuna kati ya Sh. milioni saba na milioni tisa kwa siku kupitia malipo mbalimbali wawapo nje ya nchi lakini sasa hali iko tofauti kwani safari hizo zimebaki kuwa historia.
“Anayefaidi hapa ni Mahiga tu kwa sababu maelezo ya safari zake yako wazi, yanajitosheleza kutokana na wizara anayoiongoza… hawa mawaziri wengine mambo kwao ni magumu. Wapo waliojaribu kuomba safari wakaishia kugonga mwamba kwa sababu ya kutokidhi vigezo vya kupata kibali,” chanzo kingine kiliongeza. 
MAHIGA ANAVYOFAIDI 
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa kutokana na asili ya wizara anayoiongoza, walau Balozi Mahiga amesafiri kwenda nje ya nchi mara nyingi kuliko hata Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Magufuli mwenyewe ambaye hadi sasa hajawahi kuvuka mipaka ya Tanzania.
Safari pekee ya Majaliwa kwenda nje ya nchi ilikuwa Januari 17 wakati alipokwenda kumuwakilisha Rais Magufuli kwenye mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika GaboroNe, Botswana.
Baadhi ya safari za Balozi Mahiga ni pamoja na ile aliyokwenda Kigali, Rwanda Februari 18 wakati alipokwenda kupeleka ujumbe wa Rais Magufuli kwa Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame na kisha akaenda Burundi kupeleka ujumbe kama huo kwa Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunzinza.
Januari 30, Mahiga alisafiri pia na Makamu wa Rais, Samia Suluhu, kwenda Addis Ababa, Ethiopia kumuwakilisha Rais Magufuli kwenye mkutano wa 26 wa marais wa Afrika. Wakati wa Rais Kikwete, mikutano kama hiyo ilihusisha msafara wa Rais pamoja na mawaziri wasiopungua wanne, achilia mbali maafisa wengine mbalimbali.
Hata hivyo, licha ya unafuu wa safari za nje alio nao Mahiga, chanzo kimedai kuwa hata yeye (Mahiga), kwa nafasi yake, ni kama hajasafiri kitu kulinganisha na hali ilivyokuwa hapo kabla.
“Ingekuwa kipindi cha awamu ya nne, saa hizi Mahiga angesafiri mara nyingi zaidi kuliko hivi sasa ambapo safari zake hazifiki sita… ila kwa wengine hali ni mbaya zaidi kwa sababu hakuna aliyewahi kwenda nje ya Tanzania,” chanzo kiliiambia Nipashe.
BILIONI 7/- KATIKA SIKU 100
Wakati akizungumzia siku 100 za Rais Magufuli tangu aingie Ikulu, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema Sh. Bilioni 7 zimeokolewa kwa kupiga marufuku safari holela za viongozi kwenda nje ya nchi.
WAZIRI KITWANGA AKIRI KUTOSAFIRI
Alipoulizwa kuhusu safari za nje, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, alisema yeye ni miongoni mwa wengi ambao hadi sasa hajawahi kusafiri kwenda nje ya nchi tangu aapishwe na Rais John Magufuli kushika wadhifa huo.
Alisema ameshindwa kufanya hivyo kwa sababu hajawahi kupata mwaliko au kutumwa na Rais Magufuli, kusafiri kwenda nje ya nchi.
“Mimi sijawahi kwenda kwa sababu sina shughuli za kufanya huko na wala Rais hajawahi kunituma… sasa naendaje bila kutumwa wala kuwa na mwaliko?” Alisema Kitwanga.
MWIJAGE, MWIGULU MBIONI KUSAFIRI 
Baada ya kutokwenda nje ya nchi tangu waapishwe, hatimaye Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba wanatarajiwa kusafiri kwa mara ya kwanza baada ya Rais Magufuli kuwaruhusu juzi kwenda Vietnam kujifunza mbinu za kuinua kilimo na kujenga viwanda.

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top