Akizungumza katika mikutano ya hadhara iliyofanyika Kigoma jana, Zitto alisema wamepanga kufanya makubwa katika halmashauri hiyo.
“Watu wa Kigoma wameonyesha mapenzi makubwa kwetu. Ninawashukuru sana kwa niaba ya chama chetu. Ninyi ndiyo mmetoa mbunge pekee kutoka ACT-Wazalendo na ninyi pia ndiyo mmefanya tuwe chama tawala hapa Kigoma Mjini. Naomba, kwa niaba ya ACT, niahidi kuwa Kigoma itakuwa mfano,” alisema Zitto.
Alisema wanatamani wananchi wa Kigoma Mjini wawe wa kwanza nchini kupata huduma bora za afya bure kupitia mpango maalumu wa Hifadhi ya Jamii utakaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).
Kupitia mpango huo, takribani wananchi wote 256,000 wa Kigoma Mjini watapata huduma za afya bure kwa kuchangia kiasi kidogo cha fedha.
Kuhusu mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara za mawe utakaofadhiliwa na Serikali ya Ubelgiji, alisema una lengo la kushirikisha vijana wa Kigoma.
Zitto ambaye alichaguliwa kuwa mbunge wa Kigoma Mjini Oktoba 25 mwaka jana, yuko katika ziara ya wiki mbili katika kata zote za jimbo hilo kuwashukuru wananchi kwa kuchagua chama hicho.
Katika ziara hiyo, anafuatana na Meya wa Manispaa hiyo, Hussein Juma na madiwani walioshinda katika uchaguzi huo uliovishirikisha vyama vingi vya siasa nchini.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )