Jaribio
la kutaka kumuondoa madarakani Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma
limegonga mwamba baada ya idadi ya kura zilizohitajika bungeni kushindwa
kutimia.
Wabunge
walitaka kumng’oa Rais Zuma kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Rufani
uliotolewa Alhamisi wiki iliyopita kuwa kiongozi huyo alikiuka sheria
kwa kutumia mabilioni ya fedha za umma kukarabati makazi yake binafsi.
Upigaji
kura ndani ya Bunge ulihitaji theluthi mbili ya wajumbe ili kumng’oa
kiongozi huyo. Chama tawala cha African National Congress (ANC) kina
idadi kubwa ya wabunge.
Katika
uamuzi wake, Mahakama ya Rufani iliamua kwamba Rais Zuma alikiuka
katiba kwa kushindwa kurejesha sehemu ya Sh2.4 bilioni za umma
alizotumia kukarabati makazi hayo yaliyopo eneo la Nkandla katika Mkoa
wa Kwa Zulu-Natal.
Rais Zuma alitumia fedha hizo kujenga bwawa la kuogelea, mabanda ya kuku na ng’ombe na chumba maalumu cha burudani.
Ripoti
iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Thuli
Madonsela mwaka 2014 ilifichua kuwa familia ya kiongozi huyo ilitumia
fedha hizo kinyume cha sheria. Thuli alimtaka rais kurejesha sehemu ya
fedha hizo.
Ijumaa
iliyopita, Rais Zuma aliomba msamaha kupitia luninga ya serikali, huku
akisema amesikitishwa na kusononeshwa na sakata hilo. Zuma alisema
atarejesha sehemu ya fedha anazodaiwa kuzitumia kama ilivyoagizwa na
mahakama.
Hoja
ya kutaka kumng’oa Rais Zuma iliwasilishwa bungeni na chama kikuu cha
upinzani cha Democratic Alliance (DA). Viongozi wa upinzani walidai kuwa
uongozi wake unafanya kinyume na ule wa Mwasisi wa Taifa hilo, Nelson
Mandela.
“Jacob Zuma ni maradhi ya kansa ndani ya mioyo ya raia wa Afrika Kusini. Hafai kamwe kuongoza taifa,” ulisema upinzani uliokuwa ukijibu hotuba ya rais ya Ijumaa.
Baada
ya Mahakama ya Rufani kutoa uamuzi wake , Kiongozi wa Economic Freedom
Fighters (EFF), Julius Malema alisema upinzani hautamruhusu Rais Zuma
kulihutubia tena bunge.
“Kuanzia
leo hatutamruhusu rais kuhutubia Bunge kwani tutamnyamazisha kwa nguvu.
Tutamfurusha bungeni kwa kuwa kuanzia sasa yeye siyo Rais wa Afrika
Kusini,” alisema Malema.
Vigogo
wa ANC waliomsaidia Hayati Mandela kuingia madarakani mwaka wa 1994,
wamemtaka Rais Zuma kujiuzulu ili kukiondolea fedheha chama hicho.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )