Featured
Loading...

Taarifa kuhusu uteuzi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William-Andey Lazaro Anangisye.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Prof. William-Andey Lazaro Anangisye kuwa Makamu Mkuu wa chuo hicho kuanzia  Disemba 5, 2017.

Katika taarifa iliyotolewa na chuo hicho imeeleza kuwa, Mkuu wa Chuo, Dkt. Kikwete baada ya kushauriwa na baraza la chuo lakini pia kushauriana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Magufuli amemteua Prof. Anangisye kushika nafasi hiyo ambayo ataitumikia kwa kipindi cha miaka mitano.

Prof. William Andey Anangisye alizaliwa Disemba 26, 1962 Rungwe mkoani Mbeya. Alipata elimu yake ya sekondari Sangu na Musoma kabla ya kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu Dar es Salaam mwaka 1986 kwa masomo ya Diploma. Amefundisha katika shule za sekondari Lyunga, Mkwawa na Tambaza kwa miaka 11 kuanzia mwaka 1988 hadi 1999.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama Mkufunzi Msaidizi mwaka 2000. Alipata Shahada ya Sanaa na Elimu mwaka 1992 na Shahada ya Umahiri katika Elimu 1997 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, alipata Shahda ya Uzamivu (PhD) kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh.

Baada ya kuhitimu PhD mwaka 2006, Prof. William Andey Anangisye alirejea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa Mkufunzi na kupanda hadi kuwa Mkufunzi Mwandamizi mwaka 2009 na kuwa Profesa Mshiriki (Associate Professor) mwaka 2012.

Hadi wakati wa uteuzi wake, Prof. William Andey Anangisye alikuwa Mkuu wa Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE) nafasi alioishika tangu Machi 2015.

Kabla ya hapo amewahi kutumikia nafasi za Makamu Mkuu (Elimu) wa Kitivo cha Elimu Mkwawa (MUCE) kati ya Mei 2012 hadi Machi 2015, Associate Dean (Elimu) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Shule ya Elimu 2009-2012 na pia Kaimu Mkuu Idara ya Elimu Msingi (Educational Foundation) tangu 2007-2009.

Agosti 17 mwaka huu aliteuliwa na Rais Dkt Magufuli kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Kwa miaka kadhaa ameshika nafasi mbalimbali kwenye taasisi nyingine kama vile Mjumbe wa Baraza na Mjumbe wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha, Chuo Kikuu cha Aga Khan, Mjumbe wa Seneti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha.

Prof. William Andey Anangisye ameshinda tuzo mbalimbali ikiwemo ya Mfanyakazi Bora wa Mwaka 2011 Shule ya Elimu na pia amepata udhamini  na kushirikiana na vyuo mbalimbali katika masuala ya elimu duniani.

Prof. William Andey Anangisye amefanya tafiti na kuchapisha machapisho mengi katika masuala ya elimu. Amechapisha zaidi ya makala 30 ambazo zimechapishwa katika majarida ya kimataifa na kitaifa. Chapisho lake la karibuni ni kitabu cha Fifty Years of Education in Tanzania, 1961-2011: A Historical Account and Review kilichochapishwa mwaka 2014 na Dar es Salaam University Press.

Hafla ya kumuaga Makamu Mkuu anayeondoka Prof. Mukandala na kumkaribisha Makamu Mkuu wa Chuo anayekuja itafanyika Disemba 7 katika Ukumbi wa Nkrumah kuazia saa 7 mchana.


Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top