Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inamshikilia mwanafunzi wa Shule ya
Sekondari ya Fahari iliyopo Goba kwa kosa la kukutwa na sare za Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kamanda
wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema jana Jumanne Desemba 5,2017
kuwa mwanafunzi huyo mwenye miaka 17 (jina linahifadhiwa) anayesoma
kidato cha tatu alikamatwa jirani na Benki ya CRDB maeneo ya Mbezi
jijini Dar es Salaam akiwa amevaa sare za JWTZ.
Amesema
mwanafunzi huyo akiwa amevaa sare alikuwa akivuta sigara hadharani na
kufanya vitendo visivyoendana na maadili ya askari.
Kamanda
Mambosasa amesema katika mahojiano ya awali, kijana huyo
alijitambulisha kuwa ni askari kutoka 501KJ Lugalo jijini Dar es
Salaam.
Amesema
baada ya kubanwa alikiri kupata sare hizo kwa rafiki zake na upekuzi
ulipofanywa ndani ya begi alilokuwa nalo alikutwa na kofia nyingine moja
ya jeshi hilo.
Pia, alikutwa na kitambulisho cha mtoto wa askari wa JWTZ Private Gabriel Kiwila wa 501 KJ.
Kamanda Mambosasa amesema kitambulisho hicho kilikuwa na picha ya mtoto wa askari huyo, Elia Gabriel.
"Mwanafunzi
huyo alikuwa akilazimisha kupewa huduma bure, ikiwemo kupanda gari bila
kulipa nauli akidai yeye ndiye askari," amesema Mambosasa.
Amesema uchunguzi unaendelea ili kuwapata rafiki zake ambao inasadikiwa huwa wanashirikiana kufanya uhalifu.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )