Jeshi
la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeandaa mazoezi ya pamoja ya kijeshi
kwa maofisa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Mazoezi
hayo yaliyopewa jina ‘Ushirikiano imara’ yanawashirikisha wanajeshi na
maofisa wa Serikali kutoka Tanzania, Uganda, Burundi, Kenya na Rwanda.
Mkuu
wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi, Brigedia Jenerali Alfred Kapinga
alisema jana Jumanne Desemba 5,2017 kuwa watu 300 wanashiriki wakiwamo
makamanda wa jeshi na maofisa wa juu kutoka wizara zaidi ya tatu ikiwamo
ya Katiba na Sheria.
Alisema
kwa Tanzania wanaoshiriki ni makamanda na maofisa watendaji wa Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo.
Brigedia
Jenerali Kapinga alisema kwa upande wa Tanzania washiriki ni 107 na
kwamba, mazoezi yameanza Desemba 4,2017 na yatazinduliwa Desemba
7,2017 na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.
“Mazoezi
yanafanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Kunduchi,
Dar es Salaam na yamejikita katika mambo makuu manne,” alisema.
Aliyataja
mambo hayo kuwa ni operesheni katika ulinzi wa amani; kupamba na
ugaidi; kupambana na uharamia wa aina yoyote ndani ya Bahari ya Hindi;
na majanga na maafa.
Alisema
lengo la mazoezi hayo ni kuwaandaa na kuwapa uwezo washiriki katika
kupanga na kutekeleza majukumu ya operesheni za ulinzi wa amani katika
kupambana na ugaidi, uharamia na kukabiliana na maafa.
Brigedia Jenerali Kapinga alisema mazoezi hayo ni ya siku 17.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )