Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imelipa siku saba
kuanzia jana Jeshi la Polisi nchini kupeleka mkataba walioingia baina
yao na Kampuni ya Lugumi, iliyopewa zabuni ya kufunga mashine za
kuchukua alama za vidole kwenye vituo vya Polisi vya wilaya nchi nzima.
Hadi sasa kampuni hiyo imeshalipwa asilimia 99 ya fedha, ilihali vituo vilivyofunga mashine hizo ni 14 kati ya 108.
Maagizo
ya kamati hiyo yaliyotolewa jana Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Aeshi Hilal wakati kamati hiyo ilipokutana na Jeshi hilo
kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na Mkaguzi
na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Aeshi
alisema jeshi hilo mwaka 2011 liliingia mkataba na Kampuni ya Lugumi
Enterprises kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole
katika vituo vya Polisi vya wilaya nchi nzima ambavyo viko 108.
Alisema
mkataba huo ulikuwa wa Sh bilioni 37 pamoja na kodi na kwamba hadi sasa
kampuni hiyo imeshapewa asilimia 99 ya fedha zote ili hali vituo
vilivyofungwa mashine hizo ni 14 tu, kati ya vituo vyote 108.
“Ukiangalia
kazi iliyofanywa tangu mwaka 2011 hadi leo ni kidogo na pesa hawa
kampuni wameshachukua asilimia 99, sasa tumewaagiza watuletee huo
mkataba ndani ya wiki moja walioingia na kampuni hiyo ili tuupitie,” alisema Aeshi.
Kuhusu
mali zinazokamatwa na polisi kwenye matukio mbalimbali nchini yakiwemo
ya wizi, Kamati imewaagiza CAG, Polisi na Mhakiki Mali wa Serikali
kufanya ukaguzi wa mali zote zinazokamatwa na polisi ili kuzifahamu
kuzipa thamani halisi kulingana na idadi yake.
Alisema
hivi sasa mali zinazokamatwa na polisi hazifanyiwi uhakiki kujua idadi
na thamani yake hivyo nyingi zinapotea bila kujua zilipokwenda na
nyingine ambazo kesi zake zimeisha, zinauzwa kwa bei ndogo kuliko
thamani halisi.
Kuhusu
maduka ya bidhaa ya majeshi nchini, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) limeiomba serikali idhini ya ukaguzi na utoaji mizigo ya
maduka ya jeshi bandarini ufanywe na jeshi hilo badala ya utaratibu wa
sasa ambao mzabuni ndiye anayesimamia jambo hilo.
Akizungumzia
hilo, Aeshi alisema maombi hayo ya jeshi yalitolewa wakati kamati hiyo
ilipokutana na JWTZ juzi na kuomba ukaguzi wa bidhaa zinazoagizwa kwa
ajili ya maduka yao zifanyiwe ukaguzi na wao kwani inawezekana bidhaa
zinazoingizwa zikawa nyingi au zikachanganywa na vitu vingine kwa kuwa
wao hawana dhamana ya kukagua.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Ernest
Mangu alisema jeshi hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile
uhaba wa nyumba na kwamba mikakati yao hivi sasa ni kufanya mabadiliko
na kulifanya jeshi hilo liwe la kisasa zaidi
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )