Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Sayansi na Uhandisi wa
Kompyuta (CoICT), Dk Richard Mgaya amefariki baada ya kuteketea ndani ya
gari lake jijini Dar es Salaam juzi.
Gari
la Dk Mgaya liliteketea baada ya kugongana na lori katika eneo la Mbezi
Africana, Wilaya ya Kinondoni usiku wa kuamkia juzi na kuwaka moto
uliosababisha kifo chake.
Juzi
picha mbalimbali zilisambaa zikionesha gari aina ya Toyota Prado
lililopata ajali eneo hilo la Africana baada ya kugongana na lori,
baadaye ilibainika kuwa aliyekuwa katika gari hilo ni Dk Mgaya.
Akizungumza
kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher
Fuime alisema gari la Dk Mgaya liliteketea na hata kushindwa kujulikana
dereva wa gari hilo.
Alisema
baadaye ndugu wa marehemu ndio walithibitisha kuwa gari hilo
lililoteketea na dereva aliyekuwemo ni Dk Mgaya ambaye hata hivyo naye
aliteketea ndani ya gari hilo.
“Lile
gari liliungua na hakuna kitu kilichopatikana, hata wakati polisi
wanafika eneo la tukio walikuta tayari dereva amekuwa majivu kutokana na
kuteketea kwa moto… labda baada ya kupima vinasaba ndio itathibitika
kama ilikuwa ni yeye,” alisema Kamanda Fuime.
Alisema
hata gari hilo hawakuweza kulitambua mara moja na baada ya kufuatilia
Mamlaka ya Mapato (TRA) ilibainika kuwa mmiliki wake ni Dk Mgaya.
Alisema “ndugu wa marehemu ndio wamesema kuwa ni ndugu yao.”
Dk
Mgaya alijiunga na idara hiyo miaka kadhaa iliyopita akitokea masomoni
nchini Marekani na alikuwa ni mtaalamu wa artificial intelligence.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )