Featured
Loading...

Polisi Yanasa Watu Wanaokejeli Mauaji ya Kimbari Rwanda

 
Kigali, Rwanda. Polisi wa Rwanda wameripoti kuwapo kesi 40 za hivi karibuni za wanaohusika na kueneza itikadi ya mauaji ya halaiki wakati wa wiki ya kuadhimisha mauaji ya halaiki iliyomalizika Jumatano iliyopita.

Msemaji wa polisi wa Rwanda, Celestin Twahirwa, amesema wahusika wanafanyiwa uchunguzi kuhusu tuhuma za kueneza habari mbaya zinazolenga kukanusha na kupuuza mauaji ya halaiki katika jamii zao.

“Tunaendelea kuchunguza ili kubaini watu wengine wanaochochea siasa za chuki na wale wanapinga kuwapo kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda.

Vyombo vyetu vinaendelea kuwafuatilia watu hao,” kilisema chanzo kimoja cha polisi.

Kitendo chochote cha kueneza itikadi kali juu ya mauaji ya halaiki au kukana kuwapo kwake ni kosa la jinai Rwanda.

Twahirwa alisema kesi hizo zinajumuisha matamshi ya watu ambao wanaonekana kulenga kuumiza hisia za waathirika wa mauaji ya halaiki yaliyotokea mwaka 1994 na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wengine kulazimika kukimbilia uhamishoni.

Amesema kuna wale ambao wamekana kufanyika mauaji ya halaiki dhidi ya Watutsi. Halikadhalika kumeripotiwa kesi ya mtu kusambaza sarafu ambazo hazitumiki tena ambazo zilitumika wakati wa utawala wa Grégoire Kayibanda.

Kayibanda anatambulika kama mmoja kati ya wachochezi wakuu wa mauaji ya kimbari Rwanda.

Halikadhalika polisi Rwanda wanasema wamemkamata mtu katika Wilaya ya Nyarugenge ambaye alisema kukumbuka waliouawa kwa umati mwaka 1994 ni kupoteza wakati.

Watu wenye itikadi ya mauaji ya halaiki na wanaokana mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi hujitokeza zaidi Aprili kila mwaka wakati wa kukumbuka mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 na Watutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani takriban milioni moja waliuawa katika kipindi cha siku 100.

Waziri wa zamani wa sheria wa Ufaransa Christiane Taubira ametoa wito wa kuwekwa wazi uhakika na ukweli kuhusu mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliyotokea Rwanda mwaka 1994.

Taubira ambaye ametoa heshima kwa waathirika zaidi ya laki nane waliouawa mwaka 1994 nchini Rwanda, amesema uhakika wa mauaji hayo ya kimbari unapaswa kuwekwa wazi.

Hata hivyo, Rwanda imekuwa ikisisitiza kuwa Serikali ya wakati huo ya Ufaransa ilishirikiana na watawala wa Kihutu wa Rwanda kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Kabila la Watutsi.

Hadi sasa watu kadhaa walioongoza mauaji ya kimbari ya Rwanda wametia nguvuni na kuhukumiwa katika mahakama maalumu iliyokuwa mjini Arusha, Tanzania. Mahakama hiyo kwa sasa imefungwa baada ya kumaliza kazi.

Karibu watu milioni moja wengi wao wakiwa Watutsi waliuawa katika mauaji hayo ya kimbari yaliyofanywa na Wahutu wenye misimamo mikali

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top