Diwani wa Kata ya Kiwalani, Mussa Kafana (Cuf), ameibuka mshindi katika
uchaguzi wa Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, kwa kumbwaga mpinzani
wake kwa kura nne.
Uchaguzi huo ulifanyika jana katika ukumbi wa Karimjee, baada ya
madiwani wa jiji hilo, ambao pia ni wajumbe wa Baraza la Halmashauri ya
jiji hilo kuapishwa.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Kaimu Mkurugenzi wa jiji hilo, Sarah
Yohana alisema, Kafana ameibuka mshindi kwa kura 10 huku mpinzani wake
Mariam Lulida (CCM) akipata kura sita.
“Kura zilizopigwa ni 16 na hakuna iliyoharibika. Namtangaza Mussa Kafana
kuwa Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam,” alisema Yohana.
Awali Meya wa jiji hilo, Isaya Mwita alisema, baraza hilo lina jukumu la
kuhakikisha linatekeleza majukumu yake ipasavyo na kila mjumbe kupitia
chama chake anapaswa kutoa mchango utakaoweza kulibadilisha Jiji la Dar
es Salaam.
Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Kafana aliwashukuru
wajumbe wa baraza hilo huku akiahidi kushirikiana nao bila kubagua
itikadi za vyama vyao, kwani wanafanya kazi kwa ajili ya wananchi na si
vyama vyao.
Alisema kwa sasa vyama havina nafasi bali maendeleo ya wananchi wa jiji hilo ndio muhimu.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Huduma za Sheria kutoka Ofisi ya
Rais, Tamisemi, Eustard Ngate, alisema, Halmashauri ya jiji hilo
ilishawahi kuvunjika mara mbili mwaka 1983 na mwaka 1996 kutokana na
viongozi wake kushindwa kuwajibika hivyo hawategemei hilo litokee
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )