Mkuu
wa Mkoa wa Arusha aliyeondolewa, Felix Ntibenda amekabidhi ofisi huku
akitoa neno la mwisho la kuwakaribisha Kigoma baadhi ya maofisa
waliokuwapo kwenye hafla hiyo.
“Karibuni sana Kigoma,”
ndiyo lilikuwa neno la mwisho kwa Ntibenda alilolitoa baada ya
kukabidhi ofisi kwa Mkuu wa Mkoa mpya Mrisho Gambo, hafla iliyofanyika
kwa muda mfupi.
Ntibenda aliyehamishiwa ofisi ya Waziri Mkuu, baada ya kusema neno hilo alipanda gari na kuondoka.
Kabla
ya makabidhiano,alikuwa wa kwanza kufika ofisini saa 3.30 asubuhi na
kulazimika kusubiri hadi 5.05 asubuhi, alipowasili mkuu mpya wa mkoa
Gambo aliyeapishwa Ikulu jijini Dar es Saalam juzi na Rais John
Magufuli.
Gambo
kabla ya uteuzi huo alikuwa mkuu wa wilaya ya Arusha na aliwasili
ofisini akiwa ameambatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama.
Aliingia ofisini kwake na kukutana na Ntibenda, ambapo walifanya makabadhiano na kutoka huku wakizungumza.
Makabidhiano
hayo yalifanyika haraka kwa kile ambacho kilielezwa na mkuu mpya wa
mkoa kutakiwa kusafiri kwenda Loliondo kupokea Mwenge wa Uhuru.
Katibu
Tawala, Richard Kwitega alisema Gambo baada ya makabidhiano alikuwa na
ratiba moja tu kuzungumzia mbio za Mwenge wa Uhuru ambao leo unaingia
mkoani hapa.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Gambo alisema jana alitarajia kuzungumzia mbio
za Mwenge pekee na kwamba unatarajiwa kuzindua miradi yenye thamani ya
Sh12.9 bilioni.
UVCCM wampokea Gambo
Kama
ambavyo, ilitarajiwa jana, viongozi wa UVCCM Mkoa wa Arusha wakiongozwa
na mwenyekiti wao, Lengai ole Sabaya walijitokeza katika mapokezi ya
Gambo.
Sabaya alisema wanampongeza Rais Magufuli kwa kusikiliza kilio chao na pia kumteua kijana kuongoza mkoa.
“Sisi kama UVCCM tumekuja hapa kumpongeza mkuu mpya wa mkoa na tuna imani naye sana kuwa atasaidia maendeleo ya mkoa huu,” alisema.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )