MWANDISHI/MTUNZI Saed Bin Salim
Kutokana na mapenzi ya mama aliyonayo kwangu, alipanga zamu ya kulala kitandani kwa wiki moja moja.
Ni maisha ambayo tulishayazoea, ilipokuwa ikifika zamu yangu mama analala chini,na ikifika zamu ya mama, mimi nalala chini.
Namshukuru Mungu amenijalia usingizi wa haraka, huwa nikiweka ubavu sigeuki mara mbili tayari nakuwa nimesinzia, nilipoingia kwenye neti hazikupita dakika tano tayari nikawa mbali sana kindoto, sikuweza kushtuka wala kuelewa chochote kilichoendelea kwa upande wa mama mpaka asubuhi ya saa moja niliposhtuka.
Sikushtuka kwa uwezo wangu bali ni kwa sababu ya mlango wa kutokea nje baada ya kusikia mama anauburuta kuufungua, niliamka na kukaa kwenye neti nikipikicha pikicha macho ambayo bado yalikuwa na usingizi.
“Shikamoo mama, nilimsalimia huku nikiwa naona kama maluelue mbele yangu kwa sababu ya matongo tongo ya kuamka niliyokuwa nayo pembezoni mwa ncha za macho yangu.
Mama aligeuka akaniitikia shikamoo yangu.
“umeamka baba? Aliniuliza.
“ndiyo mama nimeamka.
“vizuri mwanangu, basi toa neti uingize uvunguni kama kawaida, ukimaliza upige mswaki, kuna kiazi hapa kilibakia jana unaweza kukimalizia ili utafune chochote kisha utanifata shambani sawa?.
“Sawa mama.”
nilimuitika nikiwa natoka kwenye neti, alimalizia kufungua mlango akatoka nje kwa ajili ya kwenda shambani.
Niliamka na kuchukua kisturi kilichoko pembeni ya mlango nikanyagie ili kufikia juu ilipo neti, nilipanda nikaitoa kisha nikaikunja na kuiingiza uvunguni mwa kitanda. Nilichukua mswaki wa mti ambao nautumia kila siku na maji kidogo yaliyokuwa kwenye ndoo kwa ajili ya kunawa usoni.
Nadhani watoto wengi wamepitia katika hali hii hapa niliyokuwa nayo mimi, miongoni mwa vitu nilivyokuwa sivipendi ni kuoga, kwa ninavyokumbuka mpaka siku hiyo nilikuwa na zaidi ya mwezi mzima sijui maji yanawekwaje mwilini, ilifikia kipindi nikawa nagombana na mama yangu kwa sababu ya kuoga.
Nilimaliza kupiga mswaki nikaingia ndani, nikafunua kwenye sufuria na kukuta viazi viwili, nilivitoa vyote nikala baada ya kumaliza kula, nilimfuata mama shambani kumsaidia kulima na kupalilia baadhi ya sehemu ambazo zilipandwa viazi vitamu, mpaka ilipofika saa nne na robo tulitoka shambani kama kawaida yetu yeye akiwa amebeba viazi mimi kuni za kupikia ambazo huwa nazitafuta humo humo shambani kwa kuangalia baadhi ya sehemu zenye miti miti.
Ni kama nilivyokuwa nimezoea na kufanya siku zote, nikitua kuni nachukua vidumu naenda bombani nikirudi nasoma mpaka chakula kinapoiva, na siku hiyo nilifanya hivyo hivyo kwa kuwa nilishazoea bila kukumbushwa nafanya.
Ilipofika saa saba, mama alipanda kitandani ili apumzike japo nusu saa kabla ya kurudi tena shambani, nilimfata kitandani alipokuwa amelala na kukaa pembeni yake huku nikimuita.
“Naomba niende kumsalimia bibi kisha jioni narudi.’ Nilimwambia.
“Mwanangu unataka kukimbia kazi? mama aliniuliza kiunyonge akionekana kulemewa na usingizi.
“Hapana mama, nina wiki mbili sasa hivi sijamwona bibi, naenda kumsalimia tu nakurudi mama yangu, kesho ni Ijumaa pili nitakuwepo nyumbani na nitafanya kazi.
“Sawa mwanangu baiskeli yako si ni nzima?
“ndiyo mama.
“sawa msalimie sana
“Ok mama asante kwa kuniruhusu.”
Hakujibu, aligeuza ubavu wake akageukia sehemu ya pili akitafuta usingizi. Nilitoka nikafungua mlango na kuurudishia, nikaingia kwenye chumba kilichokuwa na baiskeli, nilitoka nayo nje nikapanda na kuanzisha safari ya kwenda kwa bibi moyoni, nikiwa na nia ya kwenda kumbana ili anambie ukweli wowote kuhusu baba au mwanaume aliyempa mama mimba mpaka nikazaliwa mimi.
Kutokana na nilivyokuwa napenda kuendesha baiskeli, sikumaliza dakika 28 tayari nilikuwa kwenye nyumba ya makuti ambayo alikuwa akiishi bibi peke yake maeneo ya matemwe zanzibar.
Niliegesha baiskeli huku nikimuita, nilimuita zaidi ya mara nne bila kuitika, nikaingia ndani bila kufanikiwa kumuona, nilijua maeneo yake yote anayopenda kuwepo kama si ndani.
Nilingiza baiskeli yangu ndani na kwenda nyuma ya nyumba kulikokuwa na mti mkubwa wa mnazi, nikajua lazima atakuwa huko na kama si huko basi ni kwenye shamba la karafuu.
Nilifanikiwa kumkuta chini ya mnazi nyuma ya nyumba akiwa anasokota mkeka, pembeni yake akiwa na jagi la maji pamoja na kikombe kikubwa, miguu yake alikuwa ameinyoosha akikazana kusokota mkeka.
nilimnyatia kwa nyuma ili nimzibe macho.
“Nishakuona mjukuu wangu huna haja ya kunyata tena.” Alisema bibi.
Nilijikuta nasema “Duh” bibi mwanga huyu” kimoyo moyo kisha nikamuuliza” umenionaje bibi wakati sijakuona kugeuza macho kama si uchawi?
“Harufu yako naijua mjukuu wangu.”
“Mmh harufu yangu?
“Ndiyo.”
“Ah hakuna lolote ndiyo maana mabibi mnaambiwaga wachawi hivi hivi, sijaona ukigeuza uso, niko nyuma yako hata kama ni harufu duh, Shikamoo bibi.”
“Marhaaba marhaaaba baba ujambo!
“Sijambo bibi.
“Mama yuko wapi!
“Yuko nyumbani amelala kasema nikusalimie sana.
“Ok sawa, niko nasuka mkeka wa harusi hapa au hutaki kunioa unaniongopea.
Niliishia kucheka bila kujibu chochote, nilimuangalia bibi anavyosuka mkeka, dakika kadhaa zilipita tukiongea vitu fulani vya kawaida kama bibi na mjukuu wake huku tukifurahi na kucheka sana.
Nilikatisha maongezi baada ya kuona tunachokiongea kinazidi kunoga wakati pointi ya msingi iliyonipeleka sijaiongea, nilimuita bibi na yeye akaniitikia kwa haraka huku akiwa analamba kidole chake kipate mate fulani ya kushikiza vizuri ukilii za kusukia mkeka.
“Bibi naomba nikuulize swali nisamehe lakini kabla ya kukuuliza.” Nilijihami.
alinyanyua jicho lake na kunitazama akanambia Uliza kisha akaendelea kusuka mkeka.
“Bibi tangu nizaliwe sijawahi kumuona baba, na sijawai kuambiwa kama amefariki au lah naomba unambie bibi kama unajua chochote kuhusu baba yangu.
Bibi baba yangu yuko wapi?
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )