MSAJILI
wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ameitisha Baraza la Vyama vya
Siasa ili kunusuru mvutano uliojitokeza kati ya Jeshi la Polisi na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Jaji
Mtungi amevitaka vyama vya siasa vilivyotangaza kufanya maandamano na
mikutano isiyo na tija nchi nzima kuacha, badala yake warudi kwenye meza
ya mazungumzo ili kuondoa tofauti zinazojitokeza.
Kauli
ya Jaji Mutungi imekuja baada ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
(UVCCM) nao kutangaza maandamano ya amani kwa ajili ya kupongeza
utendaji kazi wa Rais Dk. John Magufuli, huku Chadema kikiitisha
maandamano na mikutano isiyo na kikomo nchi nzima, ambayo imepewa jina
la Operesheni Ukuta.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Jaji Mutungi alisema
kufanyika kwa maandamano na mikutano hiyo, hakuwezi kuondoa changamoto
za kisiasa zilizopo, hivyo basi wanapaswa kukaa kwenye meza moja kwa
ajili ya kujadili tofauti zilizopo na kuzipatia ufumbuzi.
“Ninawaomba
wale wote wenye lengo la kuitisha maandamano na mikutano ya kisiasa
kuacha kwa sababu haiwezi kusaidia kuondoa changamoto zilizopo, bali
tunapaswa kukaa kwenye meza moja ya mazungumzo ili tuweze kujadili
tofauti hizo na kuzipatia majibu,” alisema Jaji Mutungi.
Aliongeza
kuwa licha ya kuwapo kwa jitihada za viongozi mbalimbali kujadili suala
hilo, lakini vyama hivyo vimeonekana bado vikiendelea na misimamo yao
ya kuitisha mikutano na maandamano yasiyo na kikomo, jambo ambao
linaweza kuleta hofu kwa wananchi.
Jaji
Mutungi alisema katika kipindi hiki ambacho wananchi wametulia, hakuna
haja ya kuwatia hofu au wasiwasi ili ionekane kuwa nchi ina ombwe kubwa
la uongozi, jambo ambalo linaweza kurudisha nyuma juhudi za kuleta
maendeleo.
Alisema
kutokana na hali hiyo, wananchi wanapaswa kuheshimu utawala bora na
kuacha kujadili mambo ambayo yanaweza kuvuruga amani, badala yake
wanapaswa kuangalia mustakabali wa taifa kwa kufanya kazi na kuleta
maendeleo.
“Wananchi
wanapaswa kuondoa hofu kuhusiana na migongano ya kisiasa inayojitokeza,
kwa sababu hakuna ombwe la uongozi, badala yake wanapaswa kufanya kazi
kwa masilahi ya taifa ili waweze kuleta maendeleo,” alisema.
Aliongeza
kuwa kutokana na hali hiyo, ameamua kuitisha mkutano wa Baraza la Vyama
vya Siasa ambalo linashirikisha vyama 22, vikiwamo CCM na Chadema
wajadili mambo mbalimbali ikiwamo migongano ya kisiasa, ili waweze
kuendesha shughuli zao kistaarabu.
Alisema mkutano huo utafanyika Agosti 29 na 30 mwaka huu ukishirikisha wadau mbalimbali.
Jaji
Mutungi alisema kutokana na hali hiyo, Agosti 26 kutakuwa na kikao cha
kuratibu mkutano huo ambao anaamini ni muhimu kwa ajili ya kuleta
maridhiano baada ya tofauti za kisiasa zilizojitokeza.
“Baraza
hili ni forum muhimu ya upatikanaji wa maridhiano ya kisiasa kama kuna
tofauti zilizojitokeza, kuliko kuitisha mikutano na maandamano yasiyo na
tija ambayo yanaweza kusababisha wananchi kupata hofu,” alisema.
Alisema
hakuna jambo lenye ugumu katika suala hilo, kwa sababu migongano
iliyopo inajadilika ikiwa ni pamoja na kupitia baadhi ya vifungu vya
kisheria kwa ajili ya kufatuta mwafaka.
Akizungumzia
suala la Chama cha Wananchi (CUF), Jaji Mutungi alisema migongano
iliyopo kwenye chama hicho anaijua, lakini kwa sasa hawezi kuzungumzia
lolote kwa sababu mkutano ujao utashirikisha vyama vyote kikiwamo CUF.
“Mimi
ni mlezi wa vyama vya siasa… CUF ni miongoni mwa watoto wangu, najua
udhaifu wa vyama vyote kikiwamo CUF hadi ubora wao, hata migongano
iliyojitokeza ndani ya chama hicho naijua, lakini kwa sasa nashindwa
kuongea lolote kwa sababu tuna mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa
ambalo litajadili mambo mbalimbali, ikiwamo suala la mgogoro wa CUF,” alisema Jaji Mutungi.
Kutokana
na hali hiyo, aliwataka wanachama wa chama hicho kuondoa hofu kwa
sababu suala hilo litapatiwa ufumbuzi kwa kuondoa tofauti zilizopo.
Jaji
Mutungi aliyesema hayo huku wafuasi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama
hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, wakidai kwenda katika ofisi yake
kumweleza mambo mbalimbali, ikiwamo ya ukiukwaji wa taratibu za kisheria
na kumwondoa kiongozi huyo kwenye nafasi yake uliofanywa na wafuasi wa
Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.
Katika
hatua nyingine, Chadema kimesema kimesikia wito wa Jaji Mutungi wa
kuitisha mazungumzo ambayo iwapo yatatawaliwa na nia njema na dhamira
safi ya kuheshimu Katiba ya nchi, yanaweza kuwa na manufaa kwa
Watanzania wote.
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkuu wa Idara
ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene, ilisema hatua
hiyo inaweza kuleta manufaa kama Jaji Mutungu hataegemea upande wa
Serikali.
“Wakati
Msajili wa Vyama akitoa kauli ya kuzuia kile anachokiita ‘kutunishiana
misuli’, Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali limeingilia vikao vya
ndani vya chama na kuzuia visiendelee. Hiyo yote ni kinyume na sheria,
taratibu na mamlaka yao.
“Mbali
na kuzuia vikao vya ndani, Jeshi la Polisi linashikilia watu
mbalimbali, wakiwamo wafuasi, mashabiki, wanachama, viongozi wetu kwa
kushiriki vikao hivyo, wakitekeleza wajibu na haki zao za kikatiba na
kisheria.
“Wakati
tunasubiri meza ya mazungumzo kupitia Baraza la Vyama, tunapenda
kusisitiza kuwa Chadema itasimama imara kuhakikisha misingi ya
demokrasia na utawala unaozingatia Katiba na sheria unafuatwa,” ilisema taarifa hiyo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )