Featured
Loading...

Rais Magufuli: TAKUKURU Chunguzeni Kampuni ya Robert Kisena (Simon Group)


RAIS John Magufuli ameutaka uongozi wa Mkoa wa Mwanza na TAKUKURU, kuhakikisha kuwa watu waliopora mali za Chama cha Ushirika cha Nyanza (NCU), wanapatikana na kuzirudisha mali hizo mara moja, huku akiitaja Kampuni ya Simon Group yenye umiliki katika kampuni za UDA na mabasi ya haraka Dar es Salaam (UDA-RT).

“RC (mkuu wa mkoa) umezungumza kwamba katika miaka yote aliyepewa alikuwa anunue kwa zaidi ya bilioni moja lakini amelipa milioni 34 tu na nasikia ni Simon Group.” alisema Rais Magufuli.

Simon Group ni kampuni iliyozaliwa na kampuni ya Simon Agency iliyoanzishwa mkoani Shinyanga na Robert Kisena, kushughulika na ununuzi na uchambuaji wa pamba karibu miaka minane iliyopita.

Kampuni hiyo ina historia ya kuingia kwenye migogoro mikubwa ya kibiashara na Vyama Vikuu vya Ushirika vya Kanda ya Ziwa, vikiwamo Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Mwanza (NCU) na Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU), ambavyo vinaidai mamilioni ya fedha kwa kukiuka mikataba mbalimbali, ikiwamo ya kukodi vinu vya kuchambulia pamba na ununuzi wa rasilimali.

Simon Agency inahusishwa pia na kununua kiwanda cha kusindika mafuta cha NCU kijulikanacho kama "New Era", na nyumba za ushirika huo kwa bei ya kutupa.

Inadaiwa kuwa, wakati kampuni hiyo iliweza kununua kiwanda hicho kwa Sh. milioni 34 tu, bei halisi ya kiwanda hicho na miundombinu yake ilikuwa zaidi ya Sh. bilioni 1.5.

Robert Simon Kisena, kwa kutaka mambo yamnyokee zaidi, mwaka 2008 alijaribu bahati yake kwa kugombea ujumbe wa Halmashauri ya Mkoa (CCM) kuwakilisha Wilaya ya Maswa, lakini hakubahatika kuchaguliwa.

Kuanzia hapo alijipambanua kama kada wa CCM na tajiri anayeibukia. Kipindi hiki kilishuhudia wafanyabiashara wengi nchini wakifadhili au wakiteuliwa kuwa makamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM ili wasiweze kuguswa na kwa biashara zao zinawiri.

Mwaka 2010, Robert Kisena, alijitosa kugombea ubunge Jimbo la Maswa Magharibi kwa tiketi ya CCM, lakini akashindwa na John Magalle Shibuda wa CHADEMA, katika uchaguzi uliojaa fujo za kila aina na umwagaji damu.

Katika hali iliyoashiria kwamba alikuwa tayari ameingia katika "pepo ya wasioguswa", alidiriki kumkata "mtama" (kumpiga ngwala hadi chini) Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Maswa, kofia na "crown" yake ikabwagwa chini na kuchaniwa sare, kwa sababu tu alitaka kumhoji kuhusiana na ghasia za uchaguzi.

Kwa dhambi hiyo kuu ya kudhalilisha dola, Robert Simon aliachwa huru bila kukamatwa wala kuchukuliwa hatua za kisheria kwa sababu alikuwa na kinga ya wakubwa, wakati Shibuda akisota mahabusu kwa kugeuziwa kibao.

Ni baada ya uchaguzi huo, Robert Kisena alipohamia Dar es Salaam kutafuta "malisho mapya", kwa wito au kwa kubebwa na "makada" wenzake wa CCM, baada ya kuthibitika anao ujasiri wa kutosha kuweza kuingia kambi ya "makada wa zama hizi wa CCM." Tazama Video:

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top