Aliyekuwa
Waziri wa Kilimo na Chakula na Kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Stephen Wassira ameomba wasaidizi wa Rais John Magufuli kumshauri
kufanya mazungumzo na viongozi wa upinzani ili kuepusha madhara
yanayoweza kutokea kutokana na maandamano yanayopangwa kufanyika
Septemba 1.
Wassira
ameeleza kuwa washauri hao wanapaswa kufanya hivyo kwani bado nafasi
hiyo ipo kuliko kuacha Rais aingie vitani na wananchi wake kwani madhara
yatawapata Watanzania wote.
“Wazungumze
ili wasimuingize Rais kupigana na watu wake kwa maana wote tutapoteza.
Kwa nini uweke askari polisi wote hao, msimweke Rais kwenye vita na watu
wake,” Wassira anakaririwa na Jambo Leo.
“Kinachohitajika
ni wasaidizi wa Rais kumshauri ili kuhakikisha kuwa tofuati zilizopo
baina yake na vyama vya upinzani haziendelei ili kuepusha madhara
yanayoweza kuzuilika, itafutwe suluhu,” aliongeza.
Akizungumzia
uamuzi wa Serikali kupiga marufuku kufanyika kwa mikutano na
maandamano, alisema kuwa tatizo linaweza kuwa ni aliyekuwa Mgombea wa
Urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.
Alisema
kuwa hii inatokana na joto la uchaguzi lililokuwepo pamoja na nia ya
Lowassa kuzunguka nchi nzima kuwashukuru wapiga kura, kungeweza kuzua
tafrani kubwa kwani alipata kura nyingi na alikuwa akidai ameshinda kwa
asilimia 62.
“Ukiwaruhusu
kufanya mikutano na ukwaambia kuwa atakayekuja kutoa shukurani ni
Lowassa, ambaye amekuwa akipinga kushindwa ni sawa na kurejesha hali ya
uchaguzi kipindi hiki,” alisema.
Alitaka Serikali kutoa elimu ya wazi kwa umma kuhusu sababu zinazopelekea kukataza kufanyika kwa mikutano ili kuweka mambo sawa.
“Kama
mimi hapa nimetaja sababu kwamba inawezakana kuwa ni Lowassa. Sasa na
wao Serikali waseme tu tunapiga marufuku mikutano na maandamano… wataje
[sababu]na kuzifafanua,” alieleza.
Hata
hivyo, Wassira aliwataka Chadema kusitisha adhma yao na kuhakikisha
wanafuata utaratibu ili kupata haki ya kufanya maandamano na mikutano
ambayo alieleza kuwa kila Katiba ya nchi duniani imeiweka, lakini bila
kufuata utaratibu haiwezi kuruhusiwa.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )