SIKU
moja baada ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kutangaza
kuiva kwa Mpango wa Serikali wa kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameonya juu ya kuwepo kwa matapeli katika
mpango huo.
Amewatahadharisha
wananchi kuwa makini na kujiepusha na matapeli wanaopita katika maeneo
yao na kuwataka wachange fedha za kuanzisha vikundi ili wapewe fedha
hizo na serikali.
Akizungumza
na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Majimoto,
Halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele mkoani Katavi jana, Waziri Mkuu
aliwataka wananchi kukaa macho na matapeli katika fedha hizo maarufu
kama mabilioni ya Rais John Magufuli.
“Serikali
bado hatujaanza kusambaza fedha hizo. Jihadharini na hao matapeli na
wezi hivyo wakija kwenye maeneo yenu wakamateni. Zoezi hilo likianza
mtajulishwa kupitia halmashauri zenu,” aliwasisitiza.
Alitoa
onyo hilo siku moja baada ya NEEC kutoa onyo kama hilo juzi kwa kusema
kumekuwa na taarifa kutoka sehemu mbalimbali nchini kuwa kuna baadhi ya
taasisi na watu binafsi wanawadanganya wananchi kuwa fedha hizo
zitapitia kwenye taasisi zao na kuwataka kujisajili nao ili waweze
kufaidika na fedha hizo, jambo ambalo si la kweli.
Katibu
Mtendaji wa Baraza hilo, Beng’i Issa alisema fedha hizo zimelenga
kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia Vyama vya Ushirika vya Akiba
na Mikopo (Saccos) na vikundi vya kifedha vya kijamii vikiwemo Vicoba
kwa ajili ya kuanzisha au kuendeleza shughuli za kiuchumi.
Mpango
huo uliobatizwa jina la Fedha za Mfuko wa Mzunguko, unalenga
kukabiliana na tatizo la mitaji kwa ajili ya kuendesha shughuli za
kiuchumi kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mijini na vijijini.
“Watu
na taasisi hizo zinazowadanganya wananchi zimekuwa zikiwatoza viwango
mbalimbali vya fedha kwa kile wanachodai ni ada ya usajili ili vikundi
hivyo vya wananchi viweze kusajiliwa na kutambuliwa kuweza kufaidika na
mamilioni hayo kwa kila kijiji,” alisema Issa.
Kwa
wakati tofauti Serikali ya Awamu ya Tano imesisitiza kuwa itakuwa macho
ili kuhakikisha fedha hizo zinafanya kazi iliyokusudiwa na kuwafikia
walengwa.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu jana alikagua mradi wa ujenzi wa Daraja la Kavuu
linalojengwa na Kampuni ya Nandra Engineering & Construction Ltd ya
Morogoro na kumtaka mkandarasi kulikamilisha haraka.
Ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa meta 85.34 wenye thamani ya Sh bilioni 2.7 unagharimiwa na serikali kwa asilimia 100.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )