WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kufukuzwa kazi na kufikishwa mahakamani
kwa watumishi wote wa sekta ya afya watakaobainika kula fedha
zinazochangwa na wananchi kwa ajili ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Pia
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Stephen pamoja na Mganga Mkuu
wa mkoa huo, Dk. John Gurisha kusimamia na kulinda fedha za CHF
zinazochangwa na wananchi na kuhakikisha zinatumika kama
zilivyokusudiwa.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Agosti 24, 2016) wakati
akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
jimbo la Kwela, Tarafa ya Mtowisa wilayani Sumbawanga.
"Kitendo
cha kula fedha zinazochangwa na wananchi kwa lengo la kupata huduma za
afya kinawafanya wakatetamaa ya kuendelea kuchangia mfuko huo. Kama wako
watumishi wenye tabia hizo waache mara moja," amesisitiza.
Mbali
na kutoa agizo hilo kwa uongozi wa mkoa wa Rukwa, pia Waziri Mkuu
amewataka wananchi kujiunga na CHF kwa sababu mfuko huo utawawezesha
kupata huduma za matibabu bure wao na familia zao katika kipindi cha
mwaka mzima.
Wakati
huo huo Waziri Mkuu amesema barabara ya kutoka Ntendo hadi Muze ye
urefu wa kilometa 85 itajengwa kwa kiwango cha lami ili iweze kupitika
kwa urahisi na kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati.
“Mimi
nilidhani mlima wa Kitonga ndio mkali kuliko yote na eneo la Sekenke
ndio linatisha zaidi!. Kumbe barabara ya kuja huku Mtowisa ndiyo
inatisha zaidi kuliko zote. Lazima tuweke lami ili iendelee kupitika kwa
urahisi zaidi,” amesema.
Akizungumzia
ombi lililotolewa na mbunge wa jimbo la Kwela, Ignas Malocha la kutaka
tarafa hiyo ya Mtowisa kuwa wilaya au halmashauri, Waziri Mkuu amesema
analichukua na kwenda kulifanyia tathmini na majibu atayapata kupitia
uongozi wa mkoa.
Malocha
alisema jimbo la Kwela linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya
miundombinu ya barabara hali inayosababisha wananchi kushindwa
kusafirisha mazao yao kwa urahisi.
Pia
aliomba ukanda huo wa bonde la mto Rukwa upandishwe hadhi na kuwa
wilaya au halmashauri ili kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi.
Kwa
upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa
Rukwa, Mhandisi Masuka Mkina ameelezea mkakati wa kuboresha miundombinu
ya barabara mkoani hapa ikiwemo ya kutoka Ntendo hadi Muze wilayani
iliyopo wilayani Sumbawanga.
Mhandisi
Mkina amesema Serikali imetenga jumla ya sh. milioni 170 kwa ajili ya
kuweka zege kwa ajili ya kurahisisha upandaji wa mlima hasa kwenye eneo
la Kizungu katika barabara ya kutoka Ntendo hadi Muze.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, AGOSTI 24, 2016.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )