Makamu
wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewataka wafanyakazi wa kiwanda
cha kuchakata gesi asilia kilichopo Madimba mkoani Mtwara wawe
wazalendo na wafanye kazi kwa bidii katika kulinda na kuutunza uwekezaji
huo mkubwa ambao serikali inautegemea katika uzalishaji wa nishati ya
umeme wakati taifa linaelekea kwenye nchi ya viwanda.
Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wafanyakazi na watendaji wa kiwanda hicho baada ya kutembelea kiwanda kwa mara ya kwanza tangu ashike wadhifa huo kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa kiwandani hapo akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Mtwara.
Amesema
kiwanda cha kuchakata gesi asilia ni hazina kubwa kwa Taifa hivyo ni
kikalindwa na kutunzwa ipasavyo kutokana na umuhimu wake katika
uzalishaji wa nishati ya umeme kwa maendeleo ya nchi.
Makamu
wa Rais pia amewashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wa kiwanda hicho
cha kuchakata gesi asilia cha Madimba na amewahakikishia kuwa serikali
itaendelea kuwajali na kuwathamini katika utendaji wao wa kazi na kwamba
serikali itahakikisha wafanyakazi wa kiwanda hicho wanapewa motisha ya
kutosha ili waongeze maradufu utendaji wao wa kazi ili malengo ya
serikali ya kuleta maendeleo kwa wananchi kupitia viwanda inatimia kwa
sababu taifa litakuwa na nishati ya umeme ya uhakika.
Makamu
wa Rais amewataka watendaji wa Shirika la Maendeleo la Petroli (TPDC)
ambalo linasimamia mradi huo kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya
kusaidia huduma za jamii katika vijiji vinavyozunguka mradi huo kila
mwaka ili wananchi waweze kuwa walinzi wa mitambo hiyo.
Akitoa
maelezo mafupi ya mradi huo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini Prof. James Mdoe amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata
gesi ya futi za ujazo milioni 210 kwa siku.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan
akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Kiwanda cha kuchakata gesi cha
Madimba Mhandisi Leonce namna gesi inavyopokelewa na kuchakatwa na
kusafirishwa kwa watumiaji.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan
akiangalia mfumo wa uendeshaji na usalama wa kiwanda cha kuchakata gesi
cha Madimba mkoani Mtwara.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )



