Mwenyekiti
wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Taifa, Augustine Mrema amewapongeza
wabunge wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kwa
kuamua kuacha kususa kuhudhuria vikao vya Bunge kushinikiza Naibu Spika,
Tulia Ackson ajiuzulu au aondolewe kwenye wadhifa huo.
Mgomo
huo ulisababisha wabunge wa Ukawa kutoshiriki kwenye Bunge la Bajeti,
jambo ambalo limesababisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha
2016/2017 ipitishwe bila wabunge wa upinzani kuijadili na kuchangia
mawazo yao bungeni.
Kwa
mujibu wa barua yake kwenda kwa Spika wa Bunge Job Ndugai, Mrema
ameeleza athari ya mgomo huo wa Ukawa kuwa ni kusababisha bajeti ya
serikali ipitishwe kwa mawazo ya upande mmoja wa chama tawala.
Aidha,
ilieleza kwamba mawazo ya wananchi kutoka kwenye majimbo yanayoongozwa
na wabunge wa Ukawa yalikosekana, hivyo kuwafanya wabunge hao kuwanyima
haki wapiga kura wao, kwa kuwakosesha uwakilishi kwenye Bunge la Bajeti.
“Bunge
la bajeti ni kikao nyeti kwa vile linajadili na kupitisha mapato na
matumizi ya serikali kwa mwaka husika, ambayo yanamhusu na kumgusa kila
mwananchi, hivyo haikuwa busara kwa wabunge wa Ukawa kususa vikao vya
Bunge la Bajeti na kuwafanya wapiga kura wao wakose uwakilishi kwenye
kikao nyeti kama hicho,” alisema.
Mrema
alisema, kuwepo kwao bungeni kungeweza kusaidia kuboresha bajeti hiyo
kutokana na michango yao ya mawazo ambayo wangeyatoa na kupata bajeti
bora zaidi kwa manufaa ya taifa.
“Sisemi
kwamba bajeti iliyopitishwa ni mbaya, lakini kuwepo kwa wabunge wa
upinzani kungesaidia kuboresha ili iwe nzuri zaidi kwa manufaa ya
wapigakura wao waliowachagua majimboni mwao,” alisema.
Alisema “Hata
kama Naibu Spika alikuwa na kasoro katika utendaji wake wa kazi, lakini
Ukawa hawakupaswa kususa vikao vya bunge hilo, badala yake wangetafuta
ufumbuzi wa suala kwa kufuata njia za kikatiba na kisheria, ikiwemo
kutumia kanuni za Bunge.”
Alisema
kwa kususa vikao vya Bunge, Ukawa wamesababisha madhara makubwa kwa
wananchi hususani wapigakura wao ambayo hawawezi kulipika na wanaweza
wakawaadhibu kwa kosa hilo kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020, kwa
sababu wananchi waliwachagua ili kwenda kuwawakilisha bungeni na si
kwenda kususia vikao vya Bunge.
“Sisi
TLP tunaona kwamba Ukawa wamedhoofisha upinzani badala ya kuimarisha
upinzani kama wenyewe wanavyodai, kwani huwezi kuimarisha upinzani kwa
kususia vikao vya Bunge hususani Bunge la Bajeti,” alisema.
Alisema
Ukawa wanapaswa kujifunza kwamba kususa vikao si mwarobaini wa kutatua
mgogoro ya kisiasa, bali migogoro ya kisiasa hutatuliwa kwa kupitia njia
za vikao na mazungumzo.
Hata
hivyo, alisema madhara yaliyopatikana kutokana na mgomo huo hayawezi
kulipika kwa sababu Bunge la Bajeti limeshapita na haliwezi kurudiwa.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )