Mbunge
wa Jimbo la Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya jana alikaliwa kooni na
mawakili wa wadai katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi 2015
wakimtaka kutoa ufafanuzi wa idadi ya wapigakura waliojiandikisha kwenye
daftari la wapiga kura.
Katika
uchaguzi mkuu wa ubunge Jimbo la Bunda Oktoba 25, 2015, Bulaya
alimbwaga mgombea wa CCM na mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira lakini
wapigakura wanne walifungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza
kupinga matokeo. Ester alikuwa mbunge wa viti maalumu CCM, lakini
alihamia Chadema na kumshinda mkongwe Wasira.
Katika
kesi hiyo ambayo vikao vyake vinafanyika mjini Musoma na ikiwa ni siku
yake ya kwanza kutetea ubunge wake, Bulaya alibanwa na mawakili wa
walalamikaji wanaopinga ushindi wake baada ya idadi ya wapiga kura
iliyoandikwa kwenye kiapo chake kuwa tofauti na iliyoandikwa na
msimamizi wa uchaguzi kwenye fomu namba 24B ya matokeo ya uchaguzi.
Bulaya
alidai idadi ya wapiga kura walioandikishwa katika fomu ya matokeo
namba 24B aliyopewa ilikuwa 69,369 lakini imetofautiana na aliyokuwa
nayo msimamizi wa uchaguzi ambayo kuna jumla ya wapiga kura 69,460 baada
ya kujumlisha kura zote.
Wakili
wa upande wa mleta maombi, Hajra Mungula alitaka kujua kutoka kwa
mbunge huyo idadi ipi sahihi kati ya ile aliyoandikiwa na msimamizi wa
uchaguzi kwa mkono baada ya kuikataa ile ya kwanza na kutangaza idadi ya
wapigakura wa wilaya nzima ya Bunda ambao ni 164,794 au ile
iliyotangazwa na msimamizi huyo.
Mbunge
huyo alidai kuwa wakati msimamizi anabadilisha idadi hiyo hakuona
takwimu sahihi wakati anaandika kwa kuwa alikuwa amekaa mbali kidogo ila
aliamini kilichokuwa kinaandikwa na msimamizi huyo ambaye ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Lucy Msofe
Wakili
huyo alitaka kujua ilikuwaje hadi akaijua idadi hiyo ya wapiga kura wa
wilaya nzima waliojiandikisha ambao ni 164,794 wakati hajui idadi ya
wapigakura katika majimbo mengine ya wilaya hiyo? Mbunge huyo alijibu
kuwa yeye aliifahamu idadi hiyo baada ya kupitia daftari la wapiga kura
kabla ya uchaguzi kuanza.
Alidai
alifahamu idadi hiyo kwa kuwa aliwahi kuwa diwani na alishakuwa
kiongozi kabla ya kuwa mbunge na kusema kuwa taarifa za idadi ya wapiga
kura kwa kawaida siyo siri.
Mbunge
huyo alieleza kuwa tofauti ya idadi ya wapiga kura 69,460 na 69,469
haikuwa sawa lakini pia haikuathiri matokeo ya uchaguzi katika jimbo
hilo wala kuathiri idadi yoyote ya wapiga kura kwa kuwa tofauti hiyo ni
ndogo sana.
Alipohojiwa
na wakili wa mleta maombi wa tatu Constantine Mutalemwa, “Ni nani
aliyeziingiza takwimu hizo zinazopishana kwenye fomu namba 24B ya
matokeo ya uchaguzi, Mbunge huyo alijibu kuwa aliyeingiza takwimu hizo
kwenye fomu namba 24B ni msimamizi wa uchaguzi.
Mawakili
wa upande wa Serikali ni Angela Lushagala na Michael Haule; Bulaya
anatetewa na Tundu Lissu huku upande wa waleta maombi watatu mawakili ni
Yasini Membe, Hajra Mwingula na Constantine Mutalemwa.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa katika mahakama hiyo chini ya Jaji Noel Chocha.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )