Featured
Loading...

Rais Magufuli Aweka Jiwe La Msingi Mradi Wa Hosteli Za Wanafunzi Katika Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam

 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 21 Oktoba, 2016 ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa mabweni 20 ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Mwezi Juni mwaka huu wakati wa sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa maktaba ya kisasa ya chuo hicho.

Wakati Rais Magufuli akiweka jiwe la msingi la mradi huo, tayari ujenzi umefikia asilimia 75 ambapo majengo 20 yaliyounganishwa kimuundo yamefikia ghorofa ya nne na ujenzi huo unaofanywa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Desemba, 2016.

Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi Rais Magufuli aliyeambatana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ameipongeza TBA na wadau wote wanaoshiriki katika ujenzi huo zikiwemo Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa hatua kubwa ya ujenzi iliyofikiwa tangu ujenzi uanze tarehe 01 Julai, 2016 na amebainisha kuwa kwa kutumia TBA mradi huo utatumia kiasi kidogo cha fedha.

"Nawapongeza sana TBA kwa kazi nzuri mliyoifanya mpaka sasa, mradi huu utatumia Shilingi Bilioni 10 tu, Wakandarasi kutoka nje walitaka kujenga mabweni haya ya wanafunzi kwa Shilingi Bilioni 100, sasa mtaona wenyewe tumeokoa Shilingi ngapi" amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli ameahidi kuwa, kwa kuwa majengo hayo yanauwezo wa kubeba ghorofa sita, Serikali itafanya utaratibu wa kutumia moja ya likizo za wanafunzi kuongeza ghorofa nyingine mbili ili kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kupata nafasi.

Kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu Dkt. Magufuli amesema Serikali imetenga Shilingi Bilioni 483 kwa mwaka huu ambapo wanafunzi takribani 93,000 wanaoendelea na masomo na wanafunzi takribani 25,000 watakaoanza masomo watapatiwa mikopo lakini ameweka bayana kuwa mikopo hiyo itatolewa kwa wanafunzi ambao wanatoka kwenye familia masikini.

Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kurekebisha dosari zilizopo katika mfumo wa utoaji wa mikopo ikiwa ni pamoja na upangaji mbaya wa wanafunzi katika vyuo, kutoa mikopo kwa upendeleo, kutozingatia sifa za mkopaji, kutoa mikopo hewa na kufungua vyuo kabla ya mikopo ya wanafunzi kutolewa na pia amewaonya wanafunzi kujiepusha na vitendo visivyofaa wakati Serikali inarekebisha dosari hizo.

"Na ndio maana wakati mwingine na wabaya wanapitia humo humo, mara fanye hivi fanyeni vile, wakati wanajua kuwa mkifanya yasiyofaa Serikali itawafukuza tu ili mkafanyie mambo yenu huko.

"Kwa sababu huwezi kuwa unahangaika kutafuta fedha za kuwapa mikopo, wakati huo huo unahitaji kujenga reli, wakati huo huo unahitaji kujenga barabara, wakati huo huo unahitaji kulipa mishahara, wakati huo huo unahitaji kutoa elimu bure, wakati huo huo Karagwe kuna njaa, wakati huo huo watu wanahitaji dawa hospitali, halafu watu wengine wanataka kukuendesha kana kwamba hela unayokusanya ni kwa ajili yao tu, ni lazima tuelewane na mimi ninataka kuwaeleza kwa dhati lazima twende katika njia iliyonyooka, ni bora uwe Rais usiye maarufu lakini utimize uliyoyaahidi, asitokee mtu wa kukuendesha, ninajua mmenielewa" amesisitiza Dkt. Magufuli.

Dkt. Magufuli ameiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kujipanga vizuri kukusanya marejesho ya mikopo kwa wote waliokopeshwa na bodi hiyo ambapo mpaka sasa bodi inadai takribani Shilingi Trilioni 2.6.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Rwekaza Mukandala amesema wakati ujenzi huo ukiendelea chuo kimetenga Shilingi Bilioni 4.5 kutoka kwenye mapato yake kwa ajili ya kununua samani ikiwa ni pamoja na vitanda vya wanafunzi na pia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itashughulikia ujenzi wa uzio, jiko na bwalo la chakula.

Hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Wabunge, Makatibu Wakuu na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

21 Oktoba, 2016

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top