Mtandao
wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania ( TSNP) umepanga kuunda kamati ya
viongozi wa serikali za vyuo vikuu ili kukutana kwa dharura na Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Joyce Ndalichako.
Pia
imepanga kuandaa tamko la kupinga tamko la mabadiliko ya vigezo
vitakavyozingatiwa katika utoaji mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu,
lililotolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Elimu Mhandisi Stella
Manyanya.
Mtandao
huo umedai kuwa, mabadiliko hayo ya vigezo yamesababisha wanafunzi
wengi kukosa mikopo huku baadhi yao kupunguziwa fedha za kujikimu.
Mkurugenzi wa Haki za Wanafunzi TSNP, Venancy Shitindi jana alisema
kuwa TSNP kwa sasa inakusanya taarifa za changamoto zinazo wakabili
wanafunzi waliokosa mikopo ili kuandaa tamko la kupinga mabadiliko hayo,
litakalo pelekwa katika Ofisi ya Rais, Waziri Mkuu na Wizara ya Elimu.
“Tumepanga
kutengeneza kamati ndogo ya viongozi kwa ajili ya kukutana kwa dharura
na waziri mwenye dhamana ya elimu ili kutoa malalamiko ya wanafunzi juu
ya vigezo vipya vilivyotolewa na wizara yake, pia tunakusanya taarifa na
kuandaa tamko tutakalolisambaza katika ofisi ya rais, wizara ya elimu
na ofisi ya waziri mkuu,” alisema.
Alidai
kuwa, mtandao huo umefanya utafiti wa vigezo vipya vilivyotajwa na
kubaini kuwa haviendani na sera ya elimu ya mwaka 2014, wala ilani ya
Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na mpango mkakati wa kitaifa wa
maendeleo kama alivyosema Mhandisi Manyanya katika taarifa yake
aliyoitoa kwa vyombo vya habari.
“Baada
ya kusoma taarifa ya Naibu Waziri Manyanya tulikwenda kuangalia sera ya
elimu ya mwaka 2014, tukakuta hakuna sehemu iliyoainisha kundi
linalostahili kupata mkopo bali imeeleza elimu itolewe bure na mikopo
itolewe kwa kila mwanafunzi. Na kwamba elimu imepewa kipaumbele cha
kuleta maendeleo katika nyanja zote haijasema kwa wanaosomea masomo ya
sayansi pekee,” alisema na kuongeza.
“Hata
mpango wa maendeleo wa miaka 5 yaani 2025, unaeleza kuwa Tanzania
inatakiwa kuwa na uchumi wa kati na kwamba imetoa kipaumbele elimu
kutolewa bure kwa nyanja zote ili wapatikane wataalamu wa fani
mbalimbali na wa kutosha.”
Hata
hivyo, taarifa iliyotolewa na Mhandisi Manyanya ilisema kuwa serikali
kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, huandaa sifa na
vigezo vya utoaji Mikopo kila mwaka ili kuendana na malengo na matarajio
yaliyopo katika mipango na mikakati ya kitaifa kama ilivyoainishwa
katika Dira ya Taifa 2025.
Na
kwamba Serikali imetoa vipaumbele katika utoaji mikopo kwa wanafunzi wa
mafunzo ya Fani za Sayansi za Tiba na Afya,Ualimu wa Sayansi na
Hisabati, Uhandisi wa Viwanda, Kilimo, Mifugo, Mafuta na Gesi Asilia,
Sayansi Asilia na Mabadiliko ya Tabianchi, Sayansi za Ardhi, Usanifu
Majengo na Miundombinu.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )