Matonya.
WAFUATILIAJI wa burudani hususan
katika Muziki wa Bongo Fleva watakuwa wanazifahamu nyimbo kama Vaileth,
Anita, Taxi Bubu na Dunia Mapito ambazo zilifanya poa katika chati na
sehemu mbalimbali za starehe. Mkali wa ngoma hizo alikuwa ni Seif Shaban
maarufu kama Matonya.
Jamaa huyu ni mmoja wa wanamuziki wakongwe
wanaoendelea kulisongesha katika gemu la muziki wa Bongo Fleva ambapo
anapoibuka na ngoma mpya huwa gumzo. Kama utakumbuka miaka miwili
iliyopita alikuwa akitesa na Ngoma ya Mule Mule aliyomshirikisha Rich
Mavoko, akafunga mwaka jana na Sugua Benchi na sasa amefungua mwaka na
ngoma mpya ya Hakijaeleweka ambapo ndani ya ‘kideo’ chake yumo muuza
nyago Gigy Money.
Gigy Money na Matonya
Juzikati Matonya alitimba ndani ya Ofisi
za Global Publishers zilizopo Bamaga-Mwenge jijini Dar na kupokelewa na
Global TV Online kisha kufanyiwa mahojiano katika Kipindi cha Exclusive
na katika makala haya anafunguka zaidi;
Matonya
Showbiz: Hongera kwa
kazi zako, lakini ujio wako safari hii upo kasi sana. Umefunga mwaka na
Sugua Benchi na umefungua na Hakijaeleweka, kwa nini umetoa ngoma haraka
hivi kwa kipindi kifupi?
Matonya: Ujue maisha
yanabadilika! Mashabiki wangu walikuwa wamemiss sana kumsikia Matonya
kila mara akiwa na nyimbo tofauti. Hivyo mipango yangu ni kuwafurahisha
kwa kutoa nyimbo nyingi na kwa haraka zaidi.
Gigy Money
Showbiz: Kuna utofauti gani kati ya Matonya wa zamani na sasa?
Matonya: Matonya wa
zamani na sasa ni watu wawili tofauti. Mfano ukiangalia video ya wimbo
wangu huu mpya wa Hakijaeleweka ni tofauti na za nyuma. Nimeonesha
maisha ya watu wengi wasivyothamini mtu wa pembeni hadi anapoondoka
(kufariki) ndo’ wanajua thamani yake. Nimeonekana nipo makaburini nasali
kwa uchungu kitu ambacho sijawahi kukifanya katika video zangu za
nyuma.
Showbiz: Unaweza kutuambia ilikukosti kiasi gani maandalizi ya hii video?
Matonya: Nashukuru
haikutukosti kiasi kikubwa video hii japo siwezi kukitaja kwa sasa
lakini kuna vitu vidogovidogo kiukweli vilitukosti kama vile kuna sehemu
za makaburini ilibidi tukodi kisha tusubirie hadi vibali yaani process
ilikuwa ndefu sana.
Matonya
Showbiz: Katika video yako kuna video queen Gigy Money ameonekana kubadilika kimavazi, sijui unaweza kutuambia ilikuwaje?
Matonya: Kikubwa
nilitaka kubadilisha mazingira ya Gigy kwa maana watu wengi wamezoea
kumuona kwenye video na nje ya video akiwa katika mavazi ya nusu utupu.
Nimejaribu kumbadilisha na kuonesha jamii kuwa ukiishi na wanawake kama
hawa wanaweza kubadilika.
Najivunia sana kwani kwa upande wa
video, Gigy ameweza kufunika kwa kiasi kikubwa kutokana na mavazi ya
heshima aliyoyavaa mwanzo hadi mwisho yaani sasa hivi kwa walioiona
video hii wakimuona Gigy alivyo wanaweza kuleta hata ng’ombe, mbuzi au
hata wakajenga ghorofa kwa ajili ya kumchumbia.
Gigy Money
Showbiz: Ugumu gani mliupata wakati mnatengeneza video?
Matonya: Dah! Ujue
wakati tunatengeneza kwanza, tulitaka Gigy adumbukizwe (azikwe) katika
kaburi lililochimbwa kwa mujibu wa ‘skripti’. Kabla ya kufanyika video,
Gigy alinipigia simu na kuniuliza nguo zipi sasa anaweza kuzikiwa nazo
lakini tukawa tumebadilisha idea hiyo na kuonesha tayari ameshazikwa na
kaburi limetengenezwa.
Showbiz: Kwa sasa nani anasimamia kazi zako za muziki?
Matonya: Namshukuru
Mungu nina mameneja watatu, wa kwanza Kapasta 4 Real, James na Hilton
ambaye yupo Nairobi kwa ajili ya kunisimamia nje ya mipaka.
Gigy Money na Mwanahabari.
Showbiz: Unazungumziaje janga la madawa ya kulevya lililowakumba wasanii wengi kwa sasa?
Matonya: Kiukweli hali
inatisha na vijana wengi wanaangamia lakini wa kuwaokoa ni sisi wasanii
pamoja na jamii. Ni lazima tushirikiane kwa pamoja kuweza kutatua janga
hili. Kama tunaweza kushirikiana katika kuingia studio na kutoa nyimbo
kali kisha kushirikiana na media basi hata hili la kuwaokoa vijana
wenzetu tukishirikiana tunaweza kuliepuka.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )