Featured
Loading...

Kiongozi wa CHADEMA Apewa Kipigo na Vijana wa CCM Kwa Kuingilia Mkutano wao

 
Katibu wa Chadema Jimbo la Sengerema, Deusdeth Mwigala juzi, alipata kipigo kutoka kwa vijana wa CCM kilichosababisha apoteze fahamu baada ya kutuhumiwa kutaka kuvuruga mkutano wa hadhara. 

Kiongozi huyo wa Chadema alikuwa akipita karibu na eneo ambalo CCM walikuwa wakiendelea na mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Kahumulo, akiwa na vipaza sauti alivyotumia kutangaza mkutano wa chama chake, kitendo kilichotafsiriwa kuwa ni kuvuruga usikivu.

Hata hivyo, katibu huyo alikana kuvuruga mkutano wa chama hicho akidai alikuwa umbali wa zaidi ya mita 200 kutoka eneo ambalo CCM ilikuwa ikiendesha mkutano.

“Wakati naendelea na kazi ya kutangaza mkutano wa Chadema nikiwa nimeongozana na makada wengine wanne na dereva, ghafla tulivamiwa na watu wa CCM na wakaanza kutushambulia,” alisema Mwigala akizungumzia tukio hilo lililotokea Kijiji cha Lubanda.

Alisema wenzake pamoja na dereva walifanikiwa kukimbia, lakini yeye alinaswa na wafuasi hao walioendelea kumshambulia kwa kipigo. 

Hata hivyo, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, James Kisinza alimtupia lawama katibu huyo wa Chadema kwa kitendo cha kupita karibu na eneo la mkutano wa CCM akitangaza mkutano wa chama chake kwa kutumia vipaza sauti na hivyo kuvuruga usikivu. 

Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilayani Sengerema, Hassan Moshi alisema wafuasi wao walichukizwa na kitendo hicho na kuamua kumuadhibu kiongozi huyo kwa madai kuwa alikuwa anavuruga mkutano wao kwa makusudi. 

“Viongozi tulilazimika kuingilia kati kumwokoa asiendelee kuadhibiwa na vijana wenye hasira, lakini ukweli ni kwamba mwenzetu alifanya kosa kwa kuingilia mkutano wa chama kingine kinyume cha sheria,” alisema Moshi. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema ofisi yake haijapokea taarifa hizo na kuahidi kuzitolea ufafanuzi baada ya kuzipokea kutoka Sengerema.

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top