Wakati
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anatarajiwa kuwahutubia wakazi wa
Kata ya Mhandu katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani, mgombea wa
chama hicho, Godfrey Misana yupo mahabusu kutokana na kukabiliwa na
shtaka la kujeruhi.
Katibu
wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Boniphace Nkobe amesema Mbowe ameambatana
na aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu.
Amesema mkutano huo pia utahudhuriwa na aliyekuwa mbuge wa Nyamagana, Ezekia Wenje na utafanyika saa kumi jioni.
Misana
(46), mgombea udiwani wa Chadema katika uchaguzi mdogo utakaofanyika
Novemba 26,2017 na kampeni meneja wake, Charles Chinjibela (37) Ijumaa
Novemba 17,2017 walipandishwa kizimbani wakidaiwa kumjeruhi meneja wa
kampeni za CCM katika kata hiyo, Thomas Warioba.
Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, mbele ya hakimu Ainawe Moshi wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 14,2017.
Akisoma
mashtaka katika shauri hilo namba 540/2017, mwendesha mashtaka wa
Jamhuri, Elizaberth Barabara alidai washtakiwa walitumia visu na mawe
kumjeruhi Warioba.
Upande wa Jamhuri uliomba Mahakama kuzuia dhamana ya washtakiwa kwa kile ilichoeleza ni kwa usalama wao.
Ombi hilo la Jamhuri limepingwa na wakili wa utetezi, Gasper Mwanaliela.
Wakili
Mwanaliela alisema dhamana ni haki ya wateja wake na kwamba, kuwanyima
kutawazuia kushiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi mdogo wa
udiwani unaotarajiwa kufanyika Novemba 26,2017.
Baada
ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Moshi alisema Mahakama
itatoa uamuzi kuhusu dhamana Novemba 21,2017. Washtakiwa walipelekwa
mahabusu.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )