Mke wa mgombea udiwani Kata ya Mhandu (Chadema), Godfrey Misana
amelazimika kupanda jukwaani kumwombea kura mume wake aliye mahabusu
kutokana na kukabiliwa na shtaka la kujeruhi.
Katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika leo Jumapili Novemba
19,2017 katika uwanja wa Shule ya Msingi Mhandu, mwanamama huyo, Rose
aliitwa jukwaani na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ili kuomba kura
kwa ajili ya mume wake.
Rose aliwaomba wakazi wa kata ya Mhandu kumpa kura mume wake ili aweze
kuwatumikia na kutatua changamoto zote zilizopo katani hapo zikiwamo za
barabara, zahanati na maji.
Misana (46), mgombea udiwani wa Chadema katika uchaguzi mdogo
utakaofanyika Novemba 26,2017 na kampeni meneja wake, Charles Chinjibela
(37) Ijumaa Novemba 17,2017 walipandishwa kizimbani
wakidaiwa kumjeruhi meneja wa kampeni za CCM katika kata hiyo, Thomas Warioba.
Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, mbele ya hakimu Ainawe Moshi
wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 14,2017. Mahakama itatoa uamuzi
kuhusu dhamana Novemba 21,2017.
Akiomba kura, Rose amemuomba Warioba ambaye ni mlalamikaji katika kesi
hiyo kuiomba Mahakama imwachie mume wake kwa kuwa amemkumbuka pamoja na
familia yake.
"Nikuombe Warioba uwaambie Mahakama wamwachie mume wangu kwa kuwa mimi
na familia yangu tumemkumbuka sana ni siku ya tano sasa hatujamuona,
kitanda kimekuwa kikubwa jamani niko chini ya miguu yako mwache mume
wangu,” alisema Rose huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza kwenye
mkutano huo.
Mbali ya Rose kuomba kura, wananchi walijitokeza na mabango
yaliyoandikwa “Hata kama upo gerezani kura tutakupa tulia hivyo hivyo."
Imeandikwa na Kalunde Jamal, Ngollo John na Johari Shani- Mwananchi
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )