Featured
Loading...

Ufafanuzi Kuhusu Sheria Mpya Ya Ttcl Kwa Vyombo Vya Habari

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) iliyotolewa kwenye magazeti ya Mwananchi na Uhuru ya tarehe 15/11/2017. Gazeti la Mwananchi liliandika, “Serikali ‘yaiua’ rasmi TTCL na gazeti la Uhuru liliandika,“TTCL ‘bye’ ‘bye’. Vichwa hivi vya habari vimewachanganya wasomaji na kuleta taharuki kwa wateja na wafanyakazi wa TTCL, wadau wa Sekta ya Mawasiliano na wananchi kwa ujumla.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewasilisha Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania katika mkutano wa Tisa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 14 Novemba, 2017 mjini Dodoma. Bunge lilijadili na kupitisha Muswada na kutungwa kuwa Sheria itakayoanzisha Shirika la Mawasiliano Tanzania. Madhumuni ya Muswada yalikuwa ni kuanzisha Shirika la Umma la Mawasiliano nchini kwa ajili ya kulinda usalama wa nchi, kukuza uchumi na kutoa huduma za mawasiliano kwa ubora unaotakiwa. Pia, kulipa Shirika la Mawasiliano jukumu la kusimamia miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano nchini.

Sheria mpya itaiwezesha TTCL kutekeleza majukumu yake kama Shirika la Mawasiliano nchini. Hizi ni jitihada za Serikali kuimarisha TTCL na sio kuiua. TTCL bado ipo na itaendelea kutekeleza majukumu yake kama Shirika la Mawailiano nchini. Shirika litaendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa ubora na ufanisi zaidi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
17 Novemba, 2017

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top