IKIWA
imepita siku moja tangu Rais John Magufuli amwagize Waziri wa Fedha na
Mipango, Dk. Philip Mpango, kuchunguza undani wa suala la umiliki wa
kampuni ya simu ya Airtel, siri zaidi kuhusiana na kile kilichofanyika
katika ‘dili’ za mauziano zimeanza kuanikwa.
Akizungumza
mjini Dodoma juzi, Rais Magufuli alimtaka Dk. Mpango kuchunguza undani
wa kampuni ya Airtel baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa kampuni hiyo
inapaswa kuwa chini ya umiliki wa Kampuni ya Simu (TTCL), ambayo ni ya
serikali. Pia Rais Magufuli alieleza wazi kuwa kuna ‘mchezo mchafu’
uliofanywa na baadhi ya watu katika suala hilo.
Kutokana
na agizo hilo la Rais Magufuli, jana, TTCL, kupitia kwa mwenyekiti wake
wa sasa wa bodi ya wakurugenzi, Omar Nundu, na Ofisa Mtendaji Mkuu,
Waziri Kindamba, iliibuka na kuanika undani wa mambo kadhaa kuhusiana na
kampuni hiyo, mojawapo ikiwa namna vigogo watano walivyoketi kwa siku
moja na kufanya uamuzi unaoibua maswali mengi kwa sasa kuhusiana na
umiliki wa kampuni ya Airtel. Kimahesabu, siku moja ina saa 24.
Alipoulizwa
jana kuhusiana na suala hilo linaloambatana na madai kwamba TTCL ndiyo
inayoimiliki Airtel Tanzania, Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Jackoson
Mbando, alisema jambo hilo hawawezi kulizungumzia kama watendaji bali
wamiliki wa hisa walio nje ya nchi ndio wenye wajibu huo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Nundu alisema chanzo
cha yote kilianzia Agosti 5, 2005, wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi
za TTCL na Celtel wakati huo na wajumbe watano ambao majina yao hakuwa
tayari kuyataja, walipokutana siku hiyo moja na kubariki uamuzi mzito
uliofikisha jambo hilo lilipo sasa.
Nundu
alisema bodi hiyo ilikuwa na watu tisa, lakini siku hiyo moja waliketi
watano kati yao na kufanya uamuzi huo mazito huku wakiongozwa na
mwenyekiti ambaye wakati huo alikuwa amekabidhiwa asilimia moja ya hisa
zilizokuwa zikimilikiwa na ‘mtu asiyejulikana’.
Nundu alisema Celnet ilianzishwa na TTCL Mei 7, 2001 kwa mtaji wa Sh. bilioni moja na thamani ya hisa ikiwa Sh. milioni moja.
Alibainisha
kuwa TTCL ilikuwa ikimiliki hisa moja huku thamani ya hisa ilikuwa Sh.
1,000 na mtu asiyejulikana alikuwa akimiliki hisa moja yenye thamani pia
ya Sh. 1,000, kuanza baishara kwa jina la Celtel.
Hata
hivyo, Nundu alisema hisa moja ya mtu asiyejulikana ikashikiliwa na
raia wa kigeni na kwamba baadaye, TTCL ilitoa bilioni tano kwa ajili ya
mtaji ili kampuni ianze kufanya kazi.
"Ilianzishwa
kampuni inaitwa Celnet…imeanzishwa na TTCL,…ikapewa masafa megawati
900. Ilipofika wakati wa kufanya kazi, ikabadilishwa na kuwa Celtel,
kampuni hii ilianzishwa na TTCL Mei 7, 2007 mtaji wake ukiwa Sh. bilioni
moja, maana yake hisa milioni moja na kila hisa ina thamani Sh. 1,000,”
alisema Nundu.
“Lakini
wanahisa wakawa wawili, TTCL yenyewe ikachukua hisa moja, mtu
asiyejulikana akachukua hisa moja, lakini akaishika raia wa kigeni. Kwa
maana hiyo, kampuni ikaanzishwa kwa fedha Sh. 2,000," alisema Nundu.
Aidha,
Nundu alisema TTCL ilitoa pia fedha zaidi ya Sh. bilioni 82 kwa ajili
ya biashara huku cha kushangaza, mtu asiyejulikana akiwa hajatoa kitu
chochote.
"Kama
si TTCL kutoa Sh. bilioni tano, hakuna ambacho kingefanyika. Hakukuwa
na uhitaji wa mwekezaji…. isitoshe TTCL iliweka Sh. bilioni 82 na ushee
kuikopesha Celtel…sasa hapo unaona ni kampuni ya TTCL," alisema Nundu.
Alisema
baadaye, raia wa kigeni aliyekuwa akishikilia hisa moja ya mtu
asiyejulikana aliikabidhi kwa Mtanzania ambaye alikuwa miongoni mwa
wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL na pia Celtel.
“Siku
ya kikao hicho, mwenyekiti wa bodi (ambaye ndiye aliyekabidhiwa hisa
hiyo moja ya mtu asiyejulikana) na wajumbe wengine watano walifanya
maamuzi (uamuzi) magumu (mgumu) ya kuirudisha hisa hiyo moja na
kuikabidhi TTCL, hivyo TTCL ikawa inamiliki Celtel kwa hisa zote kwa
asilimia 100,” alisema.
Akieleza
zaidi kuhusiana na ‘mchezo’ uliofanyika, Nundu alisema thamani ya hisa
asilimia 100 za TTCL ilikuwa Sh. bilioni moja, lakini wakakubaliana siku
hiyo kuongeza thamani ya hisa hizo hadi kufikia Sh. bilioni 50 katika
kampuni ya Celtel.
Alisema
mpaka Mei 7, 2001, hisa 999,998 zisizo na mtu ilipewa TTCL kwa sababu
ilishaweka Sh. bilioni tano, hivyo kuwa na jumla ya hisa 999,999 huku
mtu asiyejulikana akiwa bado anamiliki hisa moja.
Nundu
alisema ilipofika Novemba 27, 2001, raia wa kigeni aliyeshikilia hisa
ya mtu asiyejulikana alimpa mtu mwingine ashikilie ambaye ni Mtanzania,
na mtu huyo aliyepewa ashikilie ndiye aliyekuwa mwenyeki wa bodi ya TTCL
na Celtel.
Nundu
aliongeza kuwa baada ya hapo, zilichukuliwa Sh. bilioni 40 za TTCL na
kuwekwa katika mfuko wa Celtel kama mtaji wake, hivyo kuifanya
kumilikiwa kwa asilimia 100 kwa mtaji wa Sh. bilioni 41, huku Sh.
bilioni tisa zikiwa hazina mmiliki.
“Siku
hiyo hiyo moja, baada ya muda TTCL ikanyang’anywa hisa zake zote na
hapo ndipo tunapojiuliza uhalali wa Celtel,” alisema Nundu.
Nundu
alisema kama hiyo haitoshi, hisa hizo zilianza kugawanywa kwa watu
ambao hawapo katika mlolongo wa Celtel kutokana na ukweli kuwa wakati
huo, waliokuwa wakitambulika ni wawili tu, yaani TTCL na ‘mtu
asiyejulikana’.
Aidha,
alisema ilikubaliwa kuwa serikali ipewe asilimia 65 na ‘mtu
asiyejulikana’ apewe asimilia 35.Alisema kwa hesabu za kawaida,
haikupaswa watu wengine kugaiwa hisa kwa sababu hawakuwa na hisa tangu
awali lakini wakapewa hisa zote.
Alisema
kama haitoshi, siku hiyo hiyo ya kikao cha bodi yenye watu watano,
serikali ikapewa hisa milioni 26.650, ikiwa ni uwiano wa asilimia 65 ya
umiliki na mwingine (mtu asiyejulikana) alipewa hisa milioni 14.350,
sawa na asilimia 35.
Baada
ya hapo, alisema serikali ilichukua tena hisa milioni 10 zingine na
kumpa mwekezaji, hivyo kumfanya afikishe milioni 24.350 na kuifanya
serikali kubakiwa na hisa milioni 16.650.
Alisema uwiano huo ndio unaoendelea hadi leo na kwamba umiliki wa Celtel upo mikononi mwa Airtel ‘kimagumashi’ (kijanjaujanja).
Kadhalika,
Nundu alisema jambo la kushangaza ni kwamba ilipofika Juni 23, mwaka
jana, Airtel ilitangaza kujitoa kwenye umiliki wa TTCL ambao walikuwa
wamiliki na wameshajitoa.
Nundu
alisema baada ya kufanyika ‘mchezo’ huo, TTCL ilikopeshwa dola za
Marekani milioni 28 na kuwekewa riba ya asilimia 18 na kusababisha deni
kukua hadi kufikia Sh. bilioni 76.6.
“Mimi
na wenzangu baada ya kuja TTCL, ndiyo tukaanza kuchimba chimba ili
kujua mbivu na mbichi kwa sababu kuna mambo mazito zaidi,” alisema.
Bosi TTCL Ajilipua
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba, alisema wanachotaka kutoka kwa Airtel ni kampuni yao.
Alisema
wanaamini na kutarajia kuwa watarejeshewa kampuni yao bila kukwaruzana
na wamikili wa kampuni ya Airtel na kwamba wamejipanga kwa ushahidi wa
asilimia 100.
“Tumeamua
kujitoa sadaka za nafsi na miili yetu kwa ajili ya kutetea wanyonge
katika vita hii kubwa ya uchumi inayoongozwa na Rais Magufuli,” alisema
Kindamba.
Pia
alisema wanatarajia kufanya biashara ya huduma za simu kwa gharama
nafuu zaidi watakaporejeshewa kampuni yao na pia kuiwezesha kulipa kodi
zaidi serikalini
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )