Featured
Loading...

Serikali yamkamata Mwanasheria Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM)

Na Joel Maduka, Geita
Mwanasheria Mkuu wa Mgodi wa dhahabu wa Geita(GGM) David Nzarigo amekamatwa na serikali baada ya kudaiwa kukutwa na nyaraka za serikali .

Mwanasheria huyo amekamatwa kwa amri ya Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh,Kangi Lugola alipotembelea Mgodi huo ambapo pamoja na mambo mengine amebaini mgodi huo kuwa unaendesha shughuli zake bila kufuata sheria ya mazingira .

Akiwa katika katika ziara ya kikazi ya siku mbili Wilayani Geita,Mhe.Kangi Lugola ameagiza kukamatwa kwa mwanasheria huyo baada ya kudaiwa kukutwa na nyaraka za serikali ambazo hazijawa rasmi kutumika kutoka taasisi ya wakala wa utafiti wa jiolojia Tanzania(GST).

Hata hivyo katika hali isiyo ya kawaida na bila kutarajiwa.Mwanasheria huyo aliyekuwa akiukingia kifua mgodi huo ili usikumbane na rungu la fidia ya uharibifu wa kimazingira kama sheria inavyotamka, alijikuta akimweleza Naibu Waziri kuwa anayo ripoti ya GST aliyodai haijaeleza iwapo mgodi huo unahusika moja kwa moja kwenye uharibifu hivyo mgodi huo usibebeshwe mzigo huo.

Kutokana na hali hiyo,Naibu Waziri Lugola aliomba apatiwe ripoti hiyo ili ajiridhishe,lakini mwanasheria huyo akijibu kwa kujiamnini alimtaka kiongozi huyo wa juu kutumia mbinu zake kuipata Serikalini, lakini yeye hawezi kutoa nyaraka ya serikali, jambo lililomkasirisha Naibu Waziri wa Muungano na Mazingira na kutoa agizo la kukamatwa mara moja.

Diwani wa kata ya mtakuja Constatine Morandi ameelezea kuwa wananchi wamekuwa wakisumbuliwa muda mrefu na mgodi bila ya kupatiwa fidia na kwamba kutokana na wao kuwa ndani ya bikoni kumesababisha kutokupatiwa huduma mbali mbali za kijamii hivyo ni vyema kwa serikali wakaweka nguvu kuwasaidia wananchi hao.

Bw Abdallah Omary-Mkazi Nyamalembo alimweleza Naibu waziri kwamba wamekuwa wakiishi maisha ya mashaka kutokana na hali ilivyo ya maeneo hayo ya mgodini na kwamba mgodi ulikwisha wai kuwapatia fidia ya shilingi elfu ishirini jambo ambalo limeonekana kuwa ni udhalilishaji kwani pesa hiyo ni ndogo.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa mgodi huo Saimon Shayo,alisema kuwa eneo ambalo wananchi wamekuwa wakilalamika kuhusu suala la fidia hadi sasa kuna nyumba mbili na kwamba fidia ya kwanza walilipa kiasi cha sh,Bilion Moja na waliipatia serikali iweze kuwafidia wananchi



Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top