JEESHI la polisi nchini limefanikiwa
kumtia mbaroni kiongozi wa kundi la waasi wa Allied Democratic Forces
(ADF) wa nchini Uganda, Jamil Mukulu, ambaye amekamatiwa nchini
Tanzania.
Mukulu aliyekuwa akiongoza waasi hao
katika mauaji wa halaiki katika nchi za Uganda na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) tangu miaka ya 1990, alikamatwa nchini
Tanzania mwanzoni mwa mwezi huu akitokea mashariki mwa DRC.
Vyombo vya habari nchini Uganda vimethibitisha kutiwa mbaroni mtu huyo ambaye kundi lake linatuhumiwa kufanya mauaji ya watu 300 tangu mwezi Oktoba mwaka jana hadi sasa huko DRC.
Mukulu ametiwa mbaroni kwa ushirikiano
wa polisi wa Tanzania na wenzao wa Uganda. Hata hivyo, jeshi la Uganda
limesema kuwa haliwezi kuthibitisha kuwa mtu aliyetiwa mbaroni ni Jamil
Mukulu hadi atakapofikishwa nchini humo na kuchukuliwa vipimo vya
vinasaba vya DNA.
Kwa muda mrefu polisi ya Uganda ilikuwa
imetoa amri ya kutiwa mbaroni kiongozi huyo wa waasi wa ADF mwenye umri
wa miaka 51 kwa tuhuma za kufanya mauaji ya kigaidi na kuiomba Interpol
iisaidie kumkamata.
Mukulu aliyekuwa muumin wa kanisa Katoliki kabla ya kuhamia Uislam, alianzisha kundi hilo la ADF mnamo miaka ya 1990, kwa ajili ya kupingana na serikali ya Uganda.
Tangu hapo amekuwa akiongoza waasi
katika mapigano ambayo yamepoteza maisha ya maelfu ya raia wa Uganda na
DRC. Mukulu anakabiliwa na makosa ya ugaidi na uhaini.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema
mwaka 1998, waasi wa ADF walifanya mauaji ya kinyama ya wanafunzi 80
walipokivamia chuo kimoja magharibi mwa Uganda.
Mwezi Novemba mwaka jana waasi hao waliwaua watu zaidi ya 100 ikiwa ni mwendelezo wa mashambulizi ya kutisha Mashariki mwa DRC.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )