Polisi
mkoani Ruvuma inawashikilia waendesha bodaboda 20 Manispaa ya Songea
wanaodaiwa kumshambulia askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ)
Kikosi cha 411 KJ Ruhuwiko, kwa kupiga mawe gari alilokuwa akiendesha
baada ya kumgonga mtembea kwa miguu.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zubeir Mwombeji alisema tukio hilo lilitokea
Machi 24 saa 3.00 usiku maeneo ya Shule ya Msingi Mfaranyaki, karibu na
Kituo Kikuu cha Polisi Songea Mjini.
Mwombeji
alimtaja mwanajeshi huyo aliyejeruhiwa kwa kushambuliwa na waendesha
bodaboda kuwa ni Luten Samweli Nginila (32), ambaye amelazwa Hospitali
ya Rufani Mkoa.
Alisema
Luteni Nginila alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili na kupoteza
fahamu baada ya kushambuliwa na waendesha bodaboda, ambao walivunja kwa
mawe vioo vya gari alilokuwa akiendesha.
Aliendelea
kuwa chanzo cha tukio hilo, inadaiwa kutokea ajali maeneo ya majengo
ambako askari huyo alikuwa akiendesha gari aina ya Nissan XTRAIL
akitokea Bar ya Ramour .
Alisema
alipofika eneo la majengo, Bahati Mbero alikatisha ghafla barabarani
hivyo askari huyo kushindwa kumudu gari na kusababisha ajali.
Kufuatia
hali hiyo, waendesha bodaboda waliokuwa karibu walikusanyika kwa lengo
la kumshambulia, hali iliyomlazimu kuwasha gari kukimbia ili kuokoa
maisha.
Hata
hivyo, bodaboda hao walimkimbiza na alipofika Shule ya Msingi
Mfaranyaki tairi la gari lake lilichomoka, hivyo walimzingira na
kumshushia kipigo wakiwamo abiria watatu aliokuwa nao.
Mwombeji
aliwataja waliokuwamo ndani ya gari hilo kuwa ni Kaumbya Kateka (24)
mkazi wa Majengo, Joyce Edson (24) mkazi wa Mpambalyoto na Jackline
Mwita (22) mwanafunzi wa Chuo cha Uuguzi Peramiho. Alisema katika vurugu
hizo baadhi ya vitu vilipotea ambavyo ni mali ya askari huyo.
Vitu vilivyopotea ni simu mbili za mkononi, pochi ambayo ilikuwa imehifadhi vitambulisho mbalimbali na Sh120,00.
Alisema wanaendelea kuwabaini wengine waliohusika, taratibu za kuwafikisha mahakamani zitafuata.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )