Katika
kile kinachoonekana kuwa ni kumchokoza waziwazi Rais John Magufuli,
Ofisa wa Elimu wa Manispaa ya Kinondoni ametoa agizo la kuwataka wakuu
wote wa shule za sekondari kwenye manispaa yake kukata Sh. 1,500 kwa
kila mwanafunzi kutoka katika fedha wanazopokea kwa ajili ya uendeshaji
wa shule zao na kisha kuzipeleka kwenye manispaa hiyo.
Katika
barua ya Februari 4, 2016 iliyosambazwa kwenda kwa walimu wakuu wa
shule za sekondari za Kinondoni na Ofisa wa Elimu wa Manispaa hiyo
aitwaye Rogers Shemwelekwa, inaelezwa kuwa fedha hizo zinapaswa kutolewa
na kila mkuu wa shule ili kugharimia michuano ya sekondari,
inayoandaliwa chini ya mwavuli wa Umoja wa Michezo kwa Shule za
Sekondari Tanzania (UMISSETA). Amri iliwataka wakuu wote wa shule za
sekondari Kinondoni zikiwamo pia zinazomilikiwa na taasisi binafsi
kuwasilisha michango hiyo ifikapo Februari 28 kupitia akaunti namba
0150259059100, katika benki ya CRDB kwa jina la KMC Miscellaneous
deposit Account na stakabadhi zote zipelekwe kwa Ofisa Elimu wa
Sekondari. Michezo hiyo ya UMESSETA inatarajiwa kuanza Mei.
Uchunguzi
wa Nipashe umebaini kuwa agizo hilo linakwenda kinyume cha waraka wa
serikali kuhusu matumizi ya fedha za ruzuku zinazotolewa kila mwezi kwa
ajili ya kufanikisha utoaji wa elimu bure iliyoahidiwa na Rais Magufuli
wakati wa kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015.
Kwa
mujibu wa waraka wa kufanikisha elimu bure, fedha zilizoguswa kupitia
agizo la Ofisa Elimu wa Kinondoni zipo katika fungu la pili ambalo
lililotengewa asilimia 30 ya fedha zote za ruzuku kwa lengo la
kuziwezesha shule siyo kugharimia michezo peke yake bali pia ukaguzi na
vifaa vya kujifunzia.
Tangu
Januari mwaka huu, serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli
imekuwa ikisambaza fedha za kufanikisha utoaji wa elimu bure kwa kila
shule kuanzia msingi hadi kidato cha nne, lengo likiwa ni kuwaondolea
wananachi kero ya kukabiliana na rundo la michango kwa visingizio
mbalimbali vikiwamo vya michezo, madawati, ulinzi, uji, nembo ya shule,
majengo karatasi, maandalizi ya mitihani, umeme, maji na masomo ya ziada
marudu kama ‘tuition’. Katika mgawo wa kwanza uliotolewa Januari,
serikali iligawa Sh. bilioni 18.77 kwa ajili ya kugharimia elimu bure
nchini kote huku Rais Magufuli akionya kuwa ole wake atakayekiuka
maelekezo na kubadilisha matumizi ya fedha hizo.
Wakizungumza
na Nipashe mwishoni mwa wiki, baadhi ya walimu wakuu wa shule za
sekondari katika manispaa ya Kinondoni wamelalamikia hatua hiyo ya
kutakiwa walipe Sh. 1,500 kwa kila mwanafunzi kwa madai kuwa kufanya
hivyo ni kwenda kinyume cha agizo la Rais kuhusiana na utoaji wa elimu
bure.
Walimu
hao, kwa nyakati tofauti walisema kuwa wao hupokea fedha moja kwa moja
kutoka Hazina zikiwa zimewekewa maelekezo, lakini wanashangaa kuona
Shemwelekwa anawapa maagizo yanayokiuka maelekezo ya Hazina kwa
kuwaagiza kwamba wakishazipata, wahakikishe wanazipeleka Manispaa kwa
ajili ya kugharimia michezo, tena kwa kiwango mahsusi cha Sh. 1,500 kwa
kila mwanafunzi.
Baadhi
ya walimu wakuu walisema ingawa idadi ya wanafunzi kwa kila shule ndiyo
kigezo cha kupokea mgawo mkubwa au kidogo, lakini kwa wastani, asilimia
30 ya ruzuku wanayopewa na serikali na ambayo hujumuisha pia shughuli
za michezo na ununuaji wa vifaa vya kujifunzia huwa haifiki Sh. 600,000
kwa mwezi.
Mmoja
wa walimu alitolea mfano wa shule yenye wanafunzi 1,000, akisema kwamba
endapo wakitii agizo la Ofisa Elimu Shemwelekwa, maana yake shule ya
aina hiyo inapaswa kulipa Sh. milioni 1.5 kwa ajili ya michezo na kiasi
chote kinapaswa kulipwa kwa wakati mmoja.
Mwalimu
mwingine aliiambia Nipashe kuwa kwa ujumla, shule moja hupata wastani
wa Sh. 1,700,000 kila mwezi kugharimia elimu bure na hivyo, ikiwa fedha
hizo zitatolewa kwa wakati mmoja, maana yake uendeshaji wa shule zao
utasimama kwa mwezi mmoja kwa sababu kiasi cha fedha kitakachobaki
kitakuwa ni kidogo na kamwe hakiwezi kufanikisha utoaji wa elimu pasi na
kuhitaji michango kutoka kwa wazazi.
OFISA ELIMU AKIRI, ARUSHA MPIRA
Akizungumza
na Nipashe kuhusu barua anayodaiwa kuiandika kwenda kwa walimu wakuu wa
manispaa yake kuhusiana na makato ya Sh. 1,500 kwa kila mwanafunzi,
Shemwelekwa alianza kwa kukiri kuandika barua hiyo, lakini akakataa
kutoa maelezo zaidi kwa madai kwamba anayepaswa kuulizwa ni mkurugenzi
wa manispaa yake.
"Siwezi kuzungumza na wewe. Ukitaka maelezo zaidi nenda kamuulize Mkurugenzi wa Manispaa,'' alisema Shemwelekwa.
Hata
hivyo, alipoulizwa, Mkurugenzi wa manispaa hiyo anayetajwa kwa jina la
Kagurumjuli Titus, alisema (yeye) hana taarifa ya kuandikwa kwa barua
hiyo ambayo Nipashe inayo nakala yake.
Aidha,
Mkurugenzi huyo alisema kama walimu wakuu hawakuridhika na barua
iliyowataka kukata fedha hizo kwa kila mwanafunzi, wangepaswa kufika
kwake ili awaweke meza moja na ofisa huyo wa elimu (Shemwelekwa) na
kufikia muafaka badala ya kukimbilia kwenye chombo cha habari.
Licha
ya mkurugenzi kudai kuwa haijui barua hiyo, nakala mojawapo ambayo
Nipashe inayo inaonyesha kuwa miongoni mwa waliotumiwa nakala kwa tarifa
ni pamoja na yeye (Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni) na pia Ofisa
Elimu Mkoa wa Dar es Salaam.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )