Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepinga mpango wa madiwani wa Halmashauri ya Meru inayoongozwa na Chadema kukopeshwa magari.
Akizungumza
katika ziara ya Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Lekule Laizer wilayani
humo, Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Langaeli Akyoo alisema wameshangazwa
madiwani kukopeshwa Sh9 milioni kila mmoja, huku wananchi wakiendelea
kuteseka kwa kero mbalimbali.
Hata
hivyo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Bakari Sajini alipinga tuhuma
hizo na kueleza kuwa hakuna kikao cha madiwani kilichopitisha uamuzi
huo, lakini kinachofanyika ni madiwani kupitia posho ya Sh350,000
wanayolipwa kila mwezi kuitumia kukopa benki.
“Kama katibu wa baraza la madiwani sina hizo taarifa, ninachojua kuna madiwani wametumia posho zao kukopa benki za CRDB na NMB kulingana na mahitaji yao na jambo hili lipo nje ya halmashauri,” alisema mkurugenzi huyo.
Mbunge
wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari alipinga madai ya CCM
akieleza kuwa hataki siasa za malumbano na chama hicho katika jimbo
hilo, huku akisisitiza aachwe afanye kazi za kutatua kero za wananchi.
Awali, akielezea kero zinazowakabili wananchi, katibu wa CCM wa wilaya hiyo alisema mojawapo ni kuwapo kwa barabara mbovu.
Alisema
kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana, halmashauri hiyo ilinunua tingatinga
kwa ajili ya ukarabati wa barabara ambazo zimekuwa zikiharibika kila
wakati.
Katibu
huyo alisema baada ya uchaguzi huo Chadema ilishinda ubunge na pia
kuongoza halmashauri, lakini ilibadili matumizi ya tingatinga na kuanza
kulikodisha kwa watu binafsi.
Mkurugenzi
wa halmashauri hiyo alisema wakati anahamia alikuta nyaraka ambazo
ziliachwa na madiwani waliopita zinazotaka tingatinga hilo kujiendesha.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )