WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bw.
Mwigulu Nchemba afanye mapitio ya vitalu vyote vilivyoko katika ranchi
ya Kitengule wilayani Karagwe na kujua nani anamiliki kitalu kipi na
kama hajaendeleza kwa mujibu wa makubaliano ni vema akanyang’anywa.
Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo juzi jioni (Jumatatu, Machi 14, 2016) alipokuwa
akizungumza na wananchi wa kata ya Kihanga wilayani Karagwe ambapo
aliitaka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ifanye mapitio katika vitalu
vyote na kuangalia wamiliki ni akina nani na kukagua vibali vyao.
Pia
aliagiza wavamizi wote kuondoka katika pori la akiba la Kimisi lililoko
wilayani Karagwe ambao wanatoka nchi jirani na kuwataka warudi makwao
na wakaanze upya kutuma maombi ya kuja kuishi nchini.
“Lazima
tulinde nchi hii kwa pamoja. Pamoja na kuwa tunatambua ujirani uliopo
na uanachama wa Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki bado kuna taratibu na
kanuni ambazo ni lazima zifuatwe. Tunao utaratibu wa kutoa kibali cha
muda usiozidi miezi sita… hawezi mtu kuja akaamua kukaa tu bila kibali
na wala Mtanzania huwezi kwenda nchi jirani ukaamua kukaa tu bila
kufuata taratibu,” alisisitiza.
Akizungumzia
migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji iliyokithiri mkoani
Kagera, Waziri Mkuu alisema inasababishwa na viongozi na wananchi
kuruhusu watu wa mataifa mengine kuingia nchini bila ya kufuata
utaratibu, ambapo aliwataka wabadilike na waache tabia hiyo.
“WanaKaragwe
mmeamua kuruhusu watu wa mataifa mengine waje kufaidi rasilmali zetu.
Hapa kuna Warundi na Wanyarwanda. Je wamefikaje kama siyo ninyi
kuwaruhusu?" alihoji.
“Lazima
tushirikiane kulinda mipaka, nimeangalia mpaka wa nchi yetu kule
Misenyi naona mambo ni hovyo hovyo tu. Vitalu vingi vinamilikiwa na
wageni, kuanzia namba 1,5,7,9,10,11 na 12 na wengine hawajaendeleza
kabisa. Kwa mfano kitalu namba tano kinatumiwa kulima bangi, Wizara
mnasubiri nini kuwanyang’anya na kukirudisha kwa Watanzania?”
“Wizara
mfanye mapitio katika vitalu vyote vilivyo pembezoni mwa vijiji.
Angalieni nani anamiliki, amepewa kwa kazi ipi na kama kama hajafanya
kitu chochote basi ni vema wakabidhiwe Watanzania wenye mifugo ili
wavitumie kunenepesha mifugo yao,” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
Akifafanua
zaidi, Waziri Mkuu alisema kuna kitalu kimoja kina hekta 36,000 na
ilikubalika kuwa kitajengwa kiwanda cha kusindika nyama nyama ya ng’ombe
lakini hata hivyo hakijafanyika kitu. “Wizara mkafanye mapitio
mumpunguzie eneo huyo mmiliki ili wafugaji wa Karagwe wafuge na
kunenepesha ng’ombe wao na kisha kuuza katika kiwanda hicho.
Waziri
Mwigulu ambaye ameambatana Waziri Mkuu katika ziara hii ya siku tatu,
ameenda Karagwe leo hii kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu wakati
Waziri Mkuu akielekea wilaya ya Ngara
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )