Jaji
Mstaafu Joseph Warioba amesema uamuzi wa serikali ya awamu ya tano wa
kuanzisha mahakama itakayoshughulikia ufisadi, rushwa na uhujumu uchumi
umekuja wakati muafaka lakini amependekeza kuwa mahakama pekee haiwezi
kushughulikia suala hilo bila kushirikiana na Jeshi la Polisi na
Takukuru.
Jaji
Warioba amesema hayo leo wakati alipoalikwa Wizara ya Katiba na Sheria
kwa ajili ya kutoa maoni na mapendekezo yake kuhusiana na serikali
kuanzisha mahakama itakayoshughulikia Rushwa na wahujumu uchumi.
“Mahakama
pekee haiwezi kushughulikia ufisadi na uhujumu uchumi bila kushirikisha
vyombo vingine ambavyo ni Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa katika kuimarisha mahakama hiyo ambayo inatarajia
kuanzishwa hivi karibuni” amesema Jaji Warioba.
Wizara
ya Katiba na Sheria imeanzisha utaratibu wa kukutana na viongozi wa
zamani ambao walishawahi kuongoza wizara hiyo kwa lengo la kupata
mapendekezo, maoni na uzoefu juu ya kuanzishwa kwa mahakama.
“Leo
nimekaribishwa wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo la kubadilishana
mawazo kuhusiana na uanzishwaji wa mahakama itakayoshughulikia ufisadi,
rushwa na wale wanao hujumu uchumi, huu ni uamuzi mzuri na hizi ni
jitihada za wazi za serikali katika kupambana na rushwa”amesema Jaji Warioba.
Amesema
lengo la serikali la kuanzisha kwa mahakama hiyo ni kupambana na
ufisadi na tayari serikali ya awamu ya tano imeonyesha dhamira ya dhati
ya kuzuia mianya ya rushwa katika ukusanyaji wa mapato.
Kwa
upande wake, Waziri wa Sheria na Katiba , Dk Harrison Mwakyembe amesema
katika kipindi kifupi cha uongozi wa rais Magufuli masuala yote ya
msingi aliyoyasema wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka
jana ameshaanza kuyatekeleza.
“Uanzishwaji
wa mahakama itakayoshughulikia ufisadi na uhujumu uchumi ni miongoni
mwa vipaumbele alivyovitoa rais Magufuli wakati wa kampeni hivyo kwa
kiasi kikubwa yale yote ambayo aliahidi kipindi cha uchaguzi ameanza
kuyatekeleza”amesema Dk Mwakyembe.
Amesema
mbali na uanzishwaji wa mahakama hiyo, pia suala la katiba mpya
litashughulikiwa lakini kwa kuanza rais Magufuli ameanza na
kuwawajibisha wale wote ambao wamekiuka maadili ya kazi zao pamoja na
kuanzisha mahakama itakayoshughulikia ufisadi na uhujumu uchumi.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )